Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kuhakikisha inasimamia kikamilifu mifumo ya Kidijitali inayotumika kwenye Sekta ya Ushirika ili mifumo hiyo iweze kuwasidia wakulima na wanaushirika kwa ujumla.

Waziri Chongolo ametoa maelekezo hayo wakati akizindua Bodi ya Makamishna wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika leo Januari 30, 2026 jijini Dodoma.

Waziri Chongolo ameigiza Tume kutumia mifumo ya kidijitali katika kufanya ukaguzi kwenye vyama  vya ushirika nchini kila mwaka na hatua stahiki kuchukuliwa kwa wahusika wote wanaokiuka taratibu za kiushirika. 

Aidha, Mhe Chongolo ameielekeza Tume na vyama vya ushirika kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa kupitia Vyama hivyo ili kupata bei nzuri na kumwinua mzalishaji.

Maelekezo mengine yaliyotolewa na Mhe. Waziri wa Kilimo ni pamoja na TCDC kuhakikisha mali za vyama vya ushirika zinawekezwa ipasavyo ili ziweze kuzalisha na kusaidia kuleta maendeleo kwa wanaushirika; kutilia mkazo uadilifu, weledi na ubunifu; ujenzi wa viwanda, upatikanaji wa huduma za bima ya mazao; na huduma za matibabu na mafao ya uzeeni kwa wakulima.

Vilevile, Waziri wa Kilimo, ameitaka Kamisheni ya TCDC kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yaliyoelekezwa kutekelezwa kupitia Ushirika yanafanyiwa kazi kikamilifu ili kuimarisha Ushirika nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya TCDC iliyozinduliwa, Abdulmajid Nsekela, amesema Kamisheni iko tayari kutekeleza maagizo yaliyotolewa na waziri wa kilimo  ili kuimarisha Ushirika nchini na kuwezesha wananchi wengi zaidi kutumia Mfumo wa Ushirika kujiletea Maendeleo.