Serikali imewataka wanaushirika nchini kuwa walinzi wakuu wa amani ya Tanzania, kuchagua viongozi waadilifu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama vya ushirika ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Wito huo umetolewa leo Julia 6, 2026 na Mgeni Rasmi, Mhe. David Silinde(Mb), Naibu Waziri wa Kilimo, aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo yaliyobeba kaulimbiu ya "Ushirika kwa Dunia Yenye Amani," Mhe. Silinde amesema wanaushirika wana wajibu mkubwa wa kulinda amani ya nchi kwa kuwa ushirika hustawi katika mazingira yenye utulivu, mshikamano na ushirikiano.

"Mwaka huu tunawakumbusha wanaushirika kuwa wao ni walinzi wakuu wa amani ya taifa letu. Ushirika wenye mafanikio hujengwa katika mazingira ya amani, hivyo kila mwanaushirika anapaswa kuwa balozi wa kudumisha umoja na utulivu nchini," amesema Mhe. Silinde.

Mhe. Silinde pia ametoa onyo dhidi ya vitendo vya ubadhirifu wa mali za ushirika, akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na matumizi mabaya ya mali za wanachama.

Kadhalika, amewahimiza wanaushirika kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama vyao kwa kutambua kuwa mafanikio ya ushirika yanategemea wanachama imara wanaotekeleza wajibu wao kwa uwajibikaji na kushiriki katika maamuzi ya maendeleo ya vyama vyao.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Silinde amesema Serikali itaendelea kuisimamia na kuiendeleza Kampeni ya "Linda Ushirika, Chagua Uadilifu" inayolenga kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na uaminifu katika vyama vya ushirika nchini.

Kwa upande wake, Msajili na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema sekta ya ushirika inaendelea kupata mafanikio makubwa, ikiwemo kuongezeka kwa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika uendeshaji wa vyama vya ushirika, hatua inayoongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji.

Dkt. Ndiege amesema pamoja na mafanikio hayo, Tume itaendelea kusimamia maadili na kuhimiza uadilifu katika vyama vya ushirika ili kuhakikisha rasilimali za wanachama zinalindwa na kusimamiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi ya utawala bora.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Federation of Cooperatives (TFC), Tito Haule, amesema mchango wa ushirika katika uchumi wa taifa unaendelea kuongezeka, akibainisha kuwa mauzo ya mazao kupitia vyama vya ushirika yamefikia thamani ya shilingi trilioni nne, jambo linaloonesha kuimarika kwa sekta hiyo na kuendelea kuongeza kipato cha wakulima na wanachama wa ushirika.

Maadhimisho ya mwaka huu yamekusanya viongozi wa Serikali, viongozi wa vyama vya ushirika, wadau wa maendeleo na wanaushirika kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kutathmini mafanikio ya sekta ya ushirika na kujadili mikakati ya kuendelea kuijenga sekta hiyo kuwa chachu ya maendeleo endelevu ya Taifa.