Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuimarisha ushirikiano katika Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwenye Vyama vya Ushirika nchini.
Taasisi hizo zimesaini Hati ya Makubaliano ya Mashirikiano (MoU) kati ya TCDC na TAKUKURU Machi 25, 2026 Jijini Dodoma.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amesema Tume imesaini makubaliano hayo kwa lengo la kuondoa madhara makubwa yanayosababishwa na vitendo vya rushwa na ubadhilifu wa fedha na mali ndani ya Vyama vya Ushirika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amebainisha ushirikiano wa Taasisi hizo utahusisha Elimu na Mafunzo, Utafiti, Uchambuzi pamoja na mikakati ya matumizi bora ya Mifumo katika Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika Vyama vya Ushirika.
Aidha, ametoa wito kwa wadau na wanaushirika kuendeleza ushirikiano ili kulinda na kujenga imani ya wanaushirika.
Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Menejimenti pamoja na watumishi wa Tume na TAKUKURU katika ofisi za TCDC.




