Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amewataka wanaushirika kote nchini kuwa walinzi wa kwanza wa mali za vyama vyao kwa kuzingatia uadilifu, uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao. Amesema misingi hiyo ni muhimu katika kujenga ushirika imara utakaoleta mabadiliko chanya kwa mwanachama mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Dkt. Ndiege ametoa wito huo leo Mei 20, 2026 jijini Dar es Salaam, alipokuwa mgeni rasmi katika Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo pamoja na uzinduzi wa kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu.” Alisisitiza kuwa, “Mlinzi wa kwanza wa mali za ushirika ni mwanaushirika mwenyewe, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha mali za vyama zinalindwa kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uwazi kama kauli mbiu yetu inavyoelekeza.” Aidha, alihimiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi, kupunguza malalamiko na kudhibiti vitendo vya ubadhirifu ndani ya vyama.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abdul Mwinte ameipongeza TCDC kwa kuanzisha kampeni hiyo yenye lengo la kuimarisha maadili ndani ya ushirika, na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kulinda na kuendeleza sekta ya ushirika pamoja na kuwahamasisha wananchi kujiunga na vyama ili kunufaika na huduma za kifedha na kijamii. Akielezea mafanikio ya vyama vya ushirika mkoani humo, Mrajis Msaidizi Angela Nalimi alitaja kuongezeka kwa upatikanaji wa mitaji, masoko ya uhakika kwa mazao na bidhaa, pamoja na kuboreshwa kwa huduma kwa wanachama.

Akihitimisha, Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Dar es Salaam, Ernest Nyambo, alisisitiza kuwa mafanikio ya ushirika yanategemea nidhamu, uaminifu na ushirikiano wa wanachama wenyewe. Alieleza kuwa jukwaa hilo litaendelea kuwa kiungo muhimu cha kuwakutanisha wadau wa ushirika ili kujadili changamoto na kubuni suluhisho endelevu. “Ni wajibu wetu sote kulinda, kuendeleza na kuthamini ushirika wetu, kwani ndio nguzo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wanachama na jamii kwa ujumla,” alisisitiza Nyambo.