TCDC Yasaini Makubaliano ya Kidijitali na Mix By Yas

​Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) yamefunguliwa rasmi leo Julai 5, 2026, jijini Dodoma. Sherehe hizi huwakutanisha wanaushirika kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa lengo la kutathmini, kujadili, na kuweka mikakati ya kuimarisha sekta ya ushirika.

​Maadhimisho hayo yamefunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula), Prof. Peter L. M. Msoffe, ambaye aliwataka wanaushirika kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha sekta hiyo.

​Katika hotuba yake ya ufunguzi, Prof. Msoffe aliwasihi wanaushirika nchini kuwa makini katika kuchagua viongozi waadilifu

​"Ili sekta hii isonge mbele, ni lazima mchague viongozi waadilifu watakaolinda na kusimamia vyema mali za wanaushirika. Uaminifu ndio nguzo kuu ya maendeleo ya taifa na ya wanaushirika wenyewe," alisisitiza Prof. Msoffe.

​Aidha, Prof. Msoffe alihitimisha kwa kutoa wito maalum kwa makundi ya vijana na wanawake, akiwataka kujitokeza kwa wingi na kuwa mstari wa mbele katika kuchangamkia fursa zitokanazo na sekta ya ushirika ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi.

​Katika hatua nyingine Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imesaini Randama ya Makubaliano (MoU) na kampuni ya mawasiliano ya Mix By Yas ambapo ​makubaliano hayo yanalenga kuleta mapinduzi ya kidijitali katika sekta ya ushirika nchini kupitia ​utoaji wa Huduma za Kifedha kwa Wanaushirika, kupata ufikiaji rahisi wa mikopo na ​malipo ya Kidijitali ya mauzo ya mazao kwa wakulima.

​Zoezi hilo la utiaji saini lilishuhudiwa na kuongozwa na Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, pamoja na Mkurugenzi wa Biashara wa Mix by Yas, James Msumari.

​Maadhimisho haya ya SUD yanatarajiwa kufikia kilele chake kesho Julai 6, 2026. ambapo kinatarajiwa kupambwa na uwepo wa Mgeni Rasmi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye atatoa mwelekeo wa serikali katika kuendeleza ushirika nchini