Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amewataka wanaushirika nchini kukamilisha ununuzi wa hisa katika Benki ya Ushirika ili kufikia asilimia 51, kuwawezesha kumiliki   benki hiyo kikamilifu. 

Rai hiyo imetolewa leo Machi 27, 2026 wakati wa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Ushirika Joint Enterprise (UJE) uliofanyika jijini Dodoma.

​Mhe. Chongolo amesisitiza kuwa wanaushirika wana uwezo wa kifedha na kuelekeza kuwa asilimia 5 zilizobaki zikamilishwe mapema iwezekanavyo ili kutimiza lengo la asilimia 51.

"Ushirika ndio nguvu ya uchumi. Kupitia Benki ya Ushirika, tutaimarisha maendeleo ya vyama vyetu na kukuza uchumi wa mwanachama mmoja mmoja," amesema Mhe. Chongolo.

Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amewahimiza wanachama kutolegalega katika ununuzi wa hisa ili kutimizq adhma yao ya kumiliki benki yenye mtaji toshelevu.

Aidha, Mkurugenzi wa Benki ya Ushirika, Godfrey Ng’urah, amebainisha kuwa chombo cha UJE ndicho kitakuwa msingi wa usimamizi wa hisa hizo na kubainisha kuwa mpaka sasa vyama vimewekeza Shilingi Bilioni 19 kati ya 29 zinazohitajika.

Ushirika Joint Enterprise (UJE) ni muungano wa pamoja wa vyama vya ushirika ulioanzishwa maalum kwa ajili ya kuratibu na kusimamia uwekezaji wa wanaushirika, kulinda maslahi ya wanachama ndani ya Benki ya Ushirika na kuhakikisha usimamizi madhubuti wa hisa za pamoja.