SERIKALI YADHAMIRIA KUEREJESHA HESHIMA NA HADHI YA USHIRIKA NCHINI.

Dodoma, 06/01/2021

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, amewataka Wanaushirika kurejesha hadhi na heshima ya Ushirika nchini kwa kujenga imani ya wananchi kwenye Sekta hiyo na kuimarisha vyama vya ushirika ili viweze kuleta tija kwa wanachama na hatimaye kuijenga Tanzania yenye uchumi imara kupitia Vyama vya Ushirika.

Prof. Mkenda alikuwa akizungumza kwenye Hafla ya Kukabidhi Vitendea Kazi kwa Warajis Wasaidizi wa Vyama Vya Ushirika wa Mikoa, iliyofanyika Jijini Dodoma, leo tarehe 06/01/2021 ambapo ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kushirikiana na wadau wengine wa Ushirika kurudisha Imani ya wananchi kwenye Ushirika.

“Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kurudisha Imani ya wananchi kwenye Vyama vya Ushirika, kwa kuhakikisha dhana ya Ushirika wa hiari inajengwa na kusimamiwa na Sheria ili kuwalinda na kuwanufaisha wanaushirika, hivyo kuchangia ipasavyo katika ustawi wao na Taifa kwa ujumla,” amesema Prof. Mkenda.

 Waziri wa Kilimo amesema kuwa Serikali katika kuimarisha Ushirika inafanya Mapitio ya Sheria ya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013 ili kuondoa mapungufu yaliyokuwa yanajitokeza katika utekelezaji wa shughuli za ushirika nchini. Aidha, Serikali itaendelea kupambana na wizi na ubadhirifu unaojitokeza kwenye Vyama vya Ushirika.

“Hatutachekeana na wezi na wabadhirifu wanaovihujumu Vyama vya Ushirika, tutapambana nao ili mali ya Wanaushirika iwe salama na iwanufaishe katika kujiletea maendeleo waliyokusudia. Hata hivyo, Serikali haitaviingilia Vyama vya Ushirika vinavyofuata Sheria, Miongozo na Taratibu zilizowekwa katika uendeshaji wake,” amesema Prof. Mkenda.

Waziri wa Kilimo ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kuendelea kuimarisha usimamizi na uhamasishaji wa uanzishwaji wa Vyama vya Ushirika nchini na kuwezesha kununua magari na kompyuta kwa baadhi ya Warajis wa mikoa ikiwa ni jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha Ushirika unaimarika na unaleta manufaa kwa wananchi. Aidha, ameipongeza na kuishukuru Benki ya CRDB, kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi za maendeleo ikiwemo ya kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa watumishi wa Serikali.

Magari na kompyuta zilizonunuliwa na Tume, pamoja na kompyuta zilizotolewa na CRDB zimekabidhiwa na Waziri wa Kilimo kwa Warajis Wasaidizi wa mikoa kwa ajili ya kuimarisha shughuli za utendaji kwa lengo la kuboresha kasi ya utendaji kazi kwenye Usimamizi wa Vyama vya Ushirika

Akizungumza katika Hafla hiyo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, amesema Tume imenunua magari mapya manne (4) aina ya Nissan Double Cabin 4WD yenye thamani ya Shilingi 275,091,670/- kwa pamoja. Pia Tume imenunua kompyuta 25 pamoja na printa moja (1) zenye thamani ya Shilingi 49,050,000/- kwa ujumla; Vilevile, Tume imekabidhiwa na Benki ya CRDB jumla ya kompyuta 50 ili kurahisisha shughuli za utendaji wa majukumu yake.

Dkt. Ndiege amesema magari mapya yaliyonunuliwa yatakwenda kwenye mikoa ya Dar es Salaam,  Simiyu, Kilimanjaro na Njombe; na gari moja lililokuwa likitumika makao makuu ya Tume litakwenda kuhudumia mkoa wa Kigoma. Hivyo, jumla ya mikoa saba (7) itakuwa na magari ikiwemo mikoa ya Mtwara na Tabora.