Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) kuhakikisha inatoa mikopo yenye riba nafuu kwa Wanaushirika ili kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao na bidhaa za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Amesema Benki ya Ushirika inayomilikiwa na Wanaushirika kwa asilimia 51 imeanza ikiwa na mtaji wa Shilingi Bilioni 55 na matawi manne (4) katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Mtwara na Tabora, na Vyama vikuu vya Ushirika zaidi ya 50 vikiwa ni mawakala wa Benki hiyo ili kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa Vyama vya Ushirika.
Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo Agosti 8, 2025 wakati akifunga Maonesho ya kimataifa ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela Jijini Dodoma.
Aidha, Rais. Dkt. Samia amewataka watendaji wa Benki ya Ushirika kuwa waadilifu na kuwasaidia Wakulima hususan wanaushirika kupata mikopo .
"Mwezi Aprili mwaka huu niliongoza Uzinduzi wa Benki ya Ushirika ambayo inamilikiwa na Wanaushirika wenyewe kwa asilimia 51 na mtaji wa shilingi za kitanzania Bilioni 55, hatua inayoimarisha upatikanaji wa mitaji kwa Vyama vya Ushirika, nitoe wito kwa wafanyakazi wa Benki hii kufanya kazi kwa uadilifu na kuhakikisha wanaushirika wanapata mikopo kwa riba nafuu ili kuendeleza mnyororo wa thamani ya mazao na bidhaa za Kilimo, Mifugo na Uvuvi," amesema Mhe. Rais Samia.
Awali Dkt. Samia amezindua Maabara Kuu ya Kilimo iliyopo katika Makao Makuu ya ya Utafiti wa kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) kwaajili ya uchunguzi katika mnyonyoro mzima wa thamani katika uchunguzi wa mimea, udongo, wadudu na uchunguzi wa sumukuvu.