Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ametoa wito kwa Viongozi mbalimbali kuhakikisha wanasimamia vema Maendeleo ya Ushirika hapa nchini na kuongeza ushirikiano baina ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi.
Ameyasema hayo wakati wa akifungua Maonesho ya 32 ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika katika viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma.
"Nawahimiza Viongozi kuhakikisha mnasimamia Maendeleo ya Ushirika na Ushirikiano baina ya Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Maafisa Ugani na watafiti wa Sera, tunaamini jambo hili litatuwezesha kubadilishana na kuchangiana elimu, rasilimali, ujuzi, na mbinu bora na mifano halisi ya kuongeza tija," amesema Dkt. Mpango.
Aidha, ametoa wito kwa Wakulima, Wafugaji,Wavuvi na wananchi wote kutembelea mabanda ya maonesho hayo ili kupata fursa za Masoko, kujifunza mbinu za kisasa za Kilimo ambazo ni endelevu na zenye tija na kusambaza matokeo ya tafiti na tektnoloja bora.
Ufunguzi wa maonesho ya Nanenane umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, Watumishi wa Umma na wananchi mbalimbali wa Dodoma na Mikoa ya jirani.
Maonesho ya Wakulima yanafanyika kwa muda wa siku nane kuanzia Agosti mosi hadi Agosti 8, 2025 yakiongozwa na kauli mbiu "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo endelevu ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi".