Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Konsotia ya Bima za Kilimo (TAIC), taasisi za kifedha pamoja na wadau wa bima ya zao la tumbaku, wakishirikiana na wakuu wa wilaya za Mkoa wa Tabora, wamekubaliana kuanza mara moja zoezi la usajili wa wakulima wa tumbaku kabla ya msimu wa kilimo kuanza.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kazi kilichofanyika leo, Septemba 17, 2025 jijini Dodoma, chenye lengo la kuboresha huduma ya bima ya mazao na kuhakikisha mkulima analindwa wakati wa majanga yanayoweza kuathiri uzalishaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amesema kupitia usajili huo, takwimu za wakulima zitakusanywa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya kampuni za bima, taasisi za kifedha na wakulima wenyewe. Ameeleza kuwa takwimu hizo zitasaidia kujua idadi sahihi ya wakulima na kuwezesha uratibu bora wa huduma.

“Huu usajili tutauanza kwenye zao la tumbaku, na baadaye utafuata kwenye mazao yote yanayosimamiwa na TCDC. Tutahakikisha tunauanza kwa uharaka kabla ya msimu wa kilimo cha tumbaku kuanza,” amesema Dkt. Ndiege.

Ameongeza kuwa suala la bima kwa wakulima ni la lazima kwa sasa, kwani linawalinda wanapokumbwa na majanga, na Serikali ina muelekeo wa kuhakikisha kila mkulima anakuwa na bima ya mazao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dkt. Khamis Mkanachi amesema usajili wa wakulima ni jambo muhimu na la haraka, kwani bila zoezi hilo utambuzi na uhalali wa wakulima unabaki kuwa fumbo.

Amefafanua kuwa kukamilika kwa usajili kutasaidia kudhibiti vitendo vya wakulima wanaotorosha tumbaku, kwa kuwa mkulima atakayekopeshwa na benki kupitia chama cha ushirika atalazimika kuuza tumbaku yake kupitia chama chake, na si vinginevyo