Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia Ushirika hapa nchini na kuhakikisha Ushirika unamwinua Mkulima na mwanaushirika kujikwamua kiuchumi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Agosti 3, 2025 wakati wa Siku maalumu ya Ushirika katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika kitaifa Jijini Dodoma.

"Leo tunazungumza hapa tukiwa tumefurahi lakini tulipotoka kulikuwa kuchungu, niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kusimamia Ushirika, tuendelee kufanya uwekezaji katika Ushirika ili Ushirika uwe nyenzo muhimu ya kumuinua mwanaushirika kiuchumi," amesema Mhe. Majaliwa.

Katika kuhakikisha kuwa Ushirika unaimarika, Waziri Mkuu ameelekeza Vyama kuongeza mauzo kupitia Stakabadhi ghalani, kuendelea kuimarisha Benki ya Ushirika, kuimarisha Mifumo ya kifedha, kutumia vizuri mikopo inayotolewa kwa Wanachama na kurejesha kwa wakati ili kujiendeleza kiuchumi.

Aidha, amewataka wadau mbalimbali wa Kilimo na Ushirika kuendelea kushirikiana na Sekta ya Ushirika ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa Maendeleo ya Wakulima, Wanaushirika, Wafanyabiashara, Wavuvi na Wafugaji.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amewataka Wakulima kuanzia Sokoni na kumalizia shambani ili kujua bei za mazao Sokoni na kulima Kilimo chenye tija.