Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussen Bashe, leo tarehe 24/10/2022 amezindua Bodi mpya ya Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), uzinduzi ambao umefanyika katika Ukumbi wa Kilimo 4 Jijini Dodoma.

Kwenye uzinduzi huo Waziri amewataka Makamishina wa Tume kuibadilisha TCDC na kuifanya iwe ni ya kibiashara zaidi ikiwa inaendelea kutoa huduma kama kawaida.

"Tume wamekuwa ni watu wa kutoa huduma bila kuangalia fursa zilizopo na wanazozisimamia ambazo nataka Makamishna mtumie fursa hizo kuifanya Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuwa ni sehemu ya manufaa na faidia kwa Wanaushirika," amesema Mhe. Bashe.

Pia amewasisitiza kufanya kazi na Menejementi ya Tume kwa kufuata misingi ya uwazi na uadilifu ili kuweza kuifanya Tume kuwa ni kimbilio la watu wote kwasababu Ushirika upo kila sehemu.

"Ni jukumu letu sote kumfanya Mkulima kupata faida ya kilimo chake na ni jukumu letu sote kuhakikisha kila mkulima au mwanaushirika yeyote anakuwa na imani na Tume ya Maendeleo ya Ushirikia Tanzania," amesema Mhe. Bashe

Waziri Bashe amesema kuwa wananchi wamekuwa na fikira ambazo si sahihi kuhusu Ushirika sasa ni jukumu la Makamishna na Menejimenti ya Tume kuondoa hizo fikira mbaya kuhusu ushirika kwani Ushirika wa leo si Ushirika wa enzi zile.

Naye Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Bw. AbdulMajid Nsekela amemhakikishia Waziri Bashe kuwa watafanya kazi kwa ushirikiano na Menejimenti ya Tume hatua kwa hatua.

Bw. Nsekela amesema kuwa Bodi itasimamia vyema Tume na Ushirika wote kwa ujumla na kuhakikisha wanawafanya wananchi walio nje ya Ushirika kutamani kujiunga katika Ushirika kama fursa za kujipatia vipato.

"Ndani ya miaka mitatu tutaacha alama na tutaanza na  kufanya mabadiliko ya mtu mmoja mmoja na pia tutashirikiana na wadau wengine katika utendaji kazi zetu na tutaisimamia vizuri Tume ya Maendeleo ya Ushirikia Tanzania.

MWISHO