Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini ametoa tuzo kwa wafanyakazi Bora wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) katika Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani ambayo kwa Mkoa wa Dodoma zimefanyika leo tarehe 01/05/2023 katika viwanja vya Jamhuri Jijini Dodoma.

Akitoa Tuzo hizo zilizowahusisha pia  watumishi wengine wa Serikali na Sekta Binafsi Mhe.Sagini amewataka watumishi na waajiri wafanye kazi kwa bidii ili kuepuka migogoro katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Ndugu wafanyakazi,niwaombe muendelee kufanya kazi kwa bidii,weledi na  maarifa mkishirikiana na waajiri na Serikali katika kuhakikisha kila sehemu ya kazi Kuna utulivu na utii wa sheria ili kuondoa migogoro isiyo na tija katika utekelezaji wa majukumu yetu kwa ufanisi," amesema Mhe.Sagini.

Akiongea kwa niaba ya Wafanyakazi wenzake waliopewa Tuzo hizo Valentino Ngoda ambaye ni Afisa TEHAMA  amesema kuwa ubunifu,uchapakazi nidhamu na kujitolea ndiko kulikopelekea kuwa mmoja wa Wafanyakazi Bora wa TCDC.

Miongoni wa watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika waliopata tuzo hizo ni Valentino Ngoda (Afisa TEHAMA), Jeremiah Boniphace (Afisa Ushirika)Delius Bushegu (Katibu Muhtasi) na Albert Mwombeki ( Afisa Sheria).