Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ameonya baadhi ya Wanaushirika wasio waadilifu kuacha tabia ya kutorosha zao la Tumbaku na kuuza kwa Wanunuzi wengine wasio na Mkataba na Vyama vyao. 

Hivyo, kusababisha vyama husika kukosa mapato na kuleta changamoto za ulipaji wa madeni ya Mikopo. 

Mrajis ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kikazi kwenye kikao na Viongozi pamoja na Wanaushirika wa Chama Kikuu cha Ushirika Milambo Juni 28,2024 tarafa ya Ulyankulu , Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora.

Dkt. Ndiege amesema Wanaushirika wachache wanaouza Tumbaku kwa wanunuzi wasio na Mkataba nje ya utaratibu wa Chama cha Ushirika husika wanasababisha changamoto ya Vyama kushindwa kulipa madeni ya Mikopo ya Mabenki na hasara kwa Mnunuzi mwenye Mkataba na Chama.

“Kila Mwanaushirika awe mlinzi wa Chama chake kwa kulinda na kufuata Taratibu na maelekezo ya Ushirika, wenye tabia za kutorosha Tumbaku waache mara moja,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, Mrajis amezindua Ghala la Chama cha Ushirika Mbeta AMCOS, ghala lililogharimu kiasi cha Shillingi Millioni 46 fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya Chama hicho.

 Mrajis pia alizindua Ghala la Chama cha Ushirika Ikonongo AMCOS lililogharimu Shillingi Millioni 84 zilizotokana na Ushirikiano na Kampuni ya Wanunuzi wa Tumbaku ya Mkwawa Leaf.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa wa Tabora, Hamis Katabaya, ameshukuru juhudi za Serikali zinazoendelea katika kuinua na kukuza Sekta ya Kilimo kwa kutoa Pembejeo za Ruzuku katika zao la Tumbaku.