Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ametoa wito kwa makampuni ya watoa huduma kwenye Vyama vya Ushirika wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo wafike katika Ofisi za Tume kwajili ya kupata kibali cha kuweza kutoa huduma kwa Vyama hivyo Nchini.

Mrajis ametoa Wito huo leo tarehe 04/11/2022 alipokuwa anafungua kikao cha watoa huduma wa Ukusanyaji madeni, Bima, Sheria, Ushauri na TEHEMA kilichofanyika Katika ukumbi wa Tawi la Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Jijini Dodoma.

Dkt Ndiege amesema Vyama vya Ushirika vinahitaji watoa huduma mbalimbali hivyo ofisi za Tume ziko wazi kwa kila Mtoa Huduma anayejiweza kutoa huduma inayohitajika kwa Wanaushirika.

“Nimefungua mlango wa ushirikiano kila anayekuja ajitathimini kabla hajafika Tume kwasababu kabla hatujakupa nafasi ni lazima tutakufuatilia kujua kama unatosha kufanya kazi na Tume kwani hatushirikiani na watu ambao si waaminifu,” amesema Dkt Ndiege.

Pia Mrajis amewataka Watoa Huduma  katika Vyama vya Ushirika kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa huduma kwa wakati kwa Vyama wanavyovihudumia na kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano na Warajis Mkoa na Maafisa Ushirika.

“Kuna Watoa Huduma ni wadangayifu, wanafanya kazi bila kuzingatia taratibu; tukikugundua unatoa rushwa ili upate kazi basi wewe utakuwa huna sifa ya kufanya kazi na Vyama vya Ushirika na pia acheni kung’ang’ania  kufanya na vyama vichache, wahitaji huduma wako wengi,” amesema Ndiege

Naye Mwenyekit wa Watoa Huduma, Aidan Bangula, amemhakikishia Mrajis kuwa watafanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Vyama vya Ushirika ambazo ndiyo muongozo wao wa kufanya kazi.

Aidha, Bangula  ameishukuru Tume kwa kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara ambayo yanawajenga kuujua vizuri Ushirika na kuwapa nafasi ya kufanya kazi kwa kufuata taratibu za Ushirika katika kutekeleza majukumu yao.