Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amewataka Wanawake nchini kujiunga katika Vyama vya Ushirika ili kuwawezesha kupata Mitaji na kuanzisha biashara mbalimbali ikiwemo Viwanda vitakavyomilikiwa na Wanaushirika wenyewe.

Mkuu wa mkoa wa Tabora ametoa wito huo  tarehe 29 Juni 2022 katika siku ya pili ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) yanayofanyika  Kitaifa Mjini Tabora.

Balozi Dkt. Burian amesema  wanawake watakapojiunga katika Vyama vya Ushirika itawawezesha kupata Nguvu ya pamoja ya kiuchumi na hivyo kuchangia kwenye kuinua pato la familia na la Taifa kwa ujumla.

"Wanawake tujiungeni katika Vyama vya Ushirika bila kujali vyeo au Madaraka tuliyonayo; mimi ni mwanachama wa Chama cha Ushirika cha Arusha Women's Business SACCOS (AWIB) na kuna wanajeshi wa vyeo mbalimbali na viongozi wa ngazi tofauti wamejiunga katika ushirika hivyo kina mama wenzangu tuitumie fursa iliyoko katika Ushirika kujiletea maendeleo," amesema Dkt. Burian.

Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt  Benson Ndiege, amesema  Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imedhamiria kuwawezesha Watanzania walio wengi kujiunga na Vyama vya Ushirika vya aina mbalimbali ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kutumia fursa zinazopatikana katika Sekta mbalimbali.