Mkurugenzi wa Sekta ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Saadat Musa ametoa wito kwa Vyama vya Ushirika kutoa elimu ya Fedha kwa Wanachama na Umma kwa ujumla kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza Sekta ya Fedha mjini na Vijijini.

Ameyasema hayo akimwakilisha Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba,  Juni 29, 2023 wakati akiongea na Wanaushirika katika siiku ya Huduma za Fedha na TEHAMA katika Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane Ipuli Mjini Tabora.

Amesema Vyama vya Ushirika vina wajibu wa kuelimisha Wanachama wake ili wawe na uelewa sahihi wa elimu ya fedha, uwekezaji na huduma jumuishi za kifedha (financial inclusion). Hivyo, kuwawezesha kuimarisha mapato yao na mitaji ya Vyama vyao. .

Aidha, ametoa Rai kwa Wanaushirika kutekeleza na kukamilisha taratibu za kuanzisha Benki ya Ushirika na kuongeza kuwa Serikali kupitia Benki kuu iko tayari kutoa ushirikiano wa kuanzisha Benki hiyo kwa kutoa miongozo na taratibu za kuanzisha Benki hiyo.

Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt Benson Ndiege, amevitaka Vyama vya Ushirika ambavyo bado havijaomba Leseni ya Uendeshaji kufanya hivyo ili kuendana na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na kuepukana na adhabu.