Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Zanzibar, Khamis Simba, ametoa wito kwa Vyama vya Ushirika kutumia Tafiti za Ushirika kuongeza maarifa na kutumia mapendekezo ya Tafiti  kubuni mbinu za kuendesha Vyama kibiashara.

Wito huo umetolewa  wakati Mrajis Simba akifunga Kongamano la Tatu la Tafiti na Maendeleo ya Ushirika leo 29 Mei, 2024 lililoanza jana Mei 28, 2024 Jijini Dodoma.

Akifunga Kongamano hilo Mrajis huyo amebainisha kuwa ni wakati sasa kwa Vyama kubadili utendaji na fikra za vyama kutoka kutoa huduma pekee bali vijielekeze katika kufanya biashara ili kuongeza mapato ya Vyama na tija kwa Wanachama.

 Aidha, Mrajis Simba amepongeza jitihada za Tume ya Maendeleo ya Ushirika  Tanzania (TCDC) katika kusimamia Vyama vya Ushirika Kidijitali hasa kupitia mifumo ya TEHAMA ambayo inawezesha kuongeza uwajibikaji, uwazi pamoja na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.

Hivyo, amesema Zanzibar itaendeleza mashirikiano ili Wanaushirika wa pande zote mbili za Muungano waweze kujifunza na kunufaika na matumizi ya mifumo ya Kidigitali.

Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege amesema ili Vyama viweze kujiendesha kibiashara ni muhimu vikafanya uwekezaji katika miradi  na si kutegemea tozo pekee.