Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Songwe, Benjamin Mangwala, amewataka viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Mazao ya Mbogamboga na Matunda kuwa chachu ya kuvutia Wananchi wengi zaidi kujiunga na Vyama vya Ushirika kwa kuongeza tija na manufaa kwa kupitia uzalishaji wa Mbogamboga na matunda.
Mrajis Msaidizi ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika wa mazao ya Mbogamboga na matunda vya Mkoa wa Songwe yanayofanyika kwa siku mbili, tarehe 4 - 5 Juni, 2024 Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.
Akiongea katika Ufunguzi huo amesema Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika yamelenga kuwajengea uwezo Viongozi wa Vyama hivyo vipya vya Ushirika wa Mbogamboga na Matunda ili waweze kusimamia vizuri vyama vyao kwa lengo la kuimarisha usimamizi sambamba na kuongeza Hati Safi za utendaji wa Vyama.
“Awali mlikuwa vikundi, hivi sasa kupitia Vyama vyenu vya Ushirika mnapata fursa ya kutambulika Kisheria, kupata fursa za mikopo, fursa za masoko, mafunzo pamoja na ongezeko la uzalishaji,” amesema Mrajis Msaidizi.
Jacob Mwasambwa, Mwenyekiti wa Ushirika wa Mbogamboga na Matunda Hasamba kutoka Wilaya ya Mbozi akichangia katika mada za mafunzo hayo amesema Chama chao cha Ushirika kimefanya jitihada za uhifadhi wa Mbogamboga kwa kuzikausha ili kuhifadhi mazao hayo wakati wa mavuno mengi na kuyatumia nje ya msimu na kuongeza zaidi fursa za masoko.
Mafunzo hayo yamejikita katika masuala ya Dhana za Ushirika, Uandishi wa Vitabu, Misingi ya Ushirika, mgawanyo wa majukumu, na Haki na Wajibu wa Wanachama.
Washiriki wa mafunzo hayo wametoka Halmashauri za Ileje, Mbozi na Tunduma wanaolima nyanya, parachichi, viazi lishe, figiri, majani ya maharage.
Mafunzo hayo yamehusisha Taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya Kilimo, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).