Ushirika ni kati ya njia thabiti zinazoweza kutumika katika kupambana na umaskini nchini hususan kwa wananchi wenye kipato cha chini kwa kupunguza changamoto za kiuchumi.

Hayo yamesemwa leo Aprili 28, 2020 na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Theresia Mahongo akiwa na Waandishi wa Habari waliofika Ofisini kwake baada ya Waandishi hao kutembelea Kiwanda cha Kusindika Maziwa cha Ushirika wa Maziwa cha Ayalabe kilichopo wilayani Karatu mkoani Arusha kinachosindika maziwa ya Karatu Milk na mazao mengine yanayotokana na maziwa.

Mkuu huyo wa Wilaya ameunga mkono juhudi za Wanaushirika wa Ayalabe kwa kuwapongeza kwa jitihada walizofanya za kujiunga pamoja na kufufua upya Kiwanda hicho cha Maziwa kilichoanza uzalishaji tangu mwezi Machi 2020 baada ya kusitisha uzalishaji na shughuli za kiwanda hicho kwa muda mrefu kutokana na migogoro mbalimbali iliyokuwepo.

Pamoja na mambo mengine Mheshimiwa Mahongo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wanaushirika wa Ayalabe kusimamia kiwanda hicho kwa uadilifu ili kuzuia masuala ya ubadhilifu na uhujumu wa mali za Ushirika, na  amewataka wale wote waliohusika kuhujumu kiwanda hicho warejeshe mali walizozichukua kinyume na taratibu.

“Nitoe wito kwa Wanaushirika kuanzia Bodi, Watendaji na Wanachama wa  Ayalabe kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa Ushirika ili kuhakikisha kuwa kiwanda hiki kinarudi katika uzalishaji wa juu na kinakuwa mkombozi wa eneo letu kwa kutoa ajira, kuinua Sekta ya Ufugaji na fursa nyingine nyingi za Kiuchumi”, alisema Mahongo.

Kwa upande wake Theresia Lawrence, mfanyabiashara mwenye duka wilayani Karatu anayeuza maziwa kutoka Kiwanda cha Kusindika maziwa cha Ayalabe miongoni mwa bidhaa mbalimbali anazouza dukani kwake, amesema maziwa ya Karatu Milk ni miongoni mwa bidhaa zinazopendwa na kununuliwa kwa wingi dukani kwake.

 “Naupongeza uongozi wa Ushirika  wa Ayalabe pamoja na Serikali kwa usimamizi madhubuti uliowezesha kuwa na kiwanda kinachotengeneza maziwa Wilayani kwetu kwani imetupa urahisi wa usafirishaji wa bidhaa hii na inatupatia faida kubwa kulinganisha na maziwa kutoka mikoa mingine,” alisema Theresia.

Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Arusha, Emmanuel Sanka akieleza hali ya Ushirika mkoani hapo amesema mkoa huo una Vyama vya Ushirika 532 vyenye jumla ya wanachama 76,000. Kutokana na Uhamasishaji wa Ushirika mkoani humo wamefanikiwa kuanzisha Vyama vya Ushirika vya wasafirishaji, vyama vya walaji pamoja na kuimarisha ushirika wa mazao ya Kimkakati ikiwemo zao la Kahawa mkoani hapo