Ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye Vyama vya Ushirika unaendelea kuimarika kwa kiasi kubwa kupitia matumizi ya Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hususan usahihi wa makusanyo, uwekaji wa kumbukumbu sahihi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ushirika.

Hayo yamesemwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Dkt. Benson Ndiege wakati akifungua Kikao Kazi cha Mafunzo ya Mfumo wa Kukusanya Mapato (Enterprise Resource Management Suite) – ERMS) kwa Warajis Wasaidizi wa Mikoa kilichofanyika, Jijini Dodoma leo Alhamisi Mei14, 2020.

Katika Kikao hicho Mrajis ameeleza kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika imedhamiria kuuimarisha Ushirika nchini kwa lengo la kuhakikisha wanachama wa Vyama vya Ushirika wananufaika na mfumo wa Ushirika. Miongoni mwa hatua muhimu za kuongeza kasi ya usimamizi wa Sekta ya Ushirika na kudhibiti mianya ya ubadhirifu ambayo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini ni pamoja na kuongeza matumizi ya TEHAMA katika utendaji wa kazi kwenye Vyama vya Ushirika.

“Jukumu kubwa la Tume ya Maendeleo ya Ushirika ni kusimamia na kuhamasisha Sekta ya Ushirika. Hivyo, tutumie vyema mifumo ya TEHAMA tuliyonayo na mifumo mipya tunayoendelea kusambaza katika Ofisi za mikoa ili kuimarisha utendaji wa kazi za Ushirika,” alisema Dkt. Ndiege.

Aidha, Mrajis amesisitiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuondoa changamoto iliyokuwepo awali ya ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye Vyama vya Ushirika uliokuwa na mapungufu mengi. “Tunapokaribia kipindi cha msimu wa mavuno ya mazao ambapo mfumo wa Stakabadhi ya Ghala utatumika katika maeneo mengi hususan kwenye mazao ya Kimkakati (Pamba, Korosho, tumbaku, kahawa, Chai) pamoja na mazao ya ufuta na Choroko, TEHAMA inakwenda kusaidia ukusanyaji wa mapato na kuweka  kumbukumbu sahihi kwa Vyama vya Ushirika,” alisema Mrajis.

Dkt. Ndiege amewaagiza Warajis Wasaidizi kusimamia kwa karibu Vyama Vikuu vya Ushirika (UNION) katika mikoa yao kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa Vyama vya Msingi vya Mazao (AMCOS) na amewataka Warajis Wasaidizi wawe mstari wa mbele kufuatilia na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika Vyama hivyo ili kubaini pale changamoto zinazojitokeza na kuweza kuzitatua mapema kwa maslahi ya wanachama wa Vyama vya Ushirika.

Kwa Upande wake Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya Anjella Maganga ametumia fursa hiyo kumpongeza Mrajis kwa hatua ya kuimarisha na kuendeleza Ushirika ngazi ya mikoa; ambapo amesema mafunzo  hayo kuhusu makusanyo ya mapato yanaenda kuwa chachu kwa Warajis Wasaidizi pamoja na Maafisa Ushirika kutekeleza wajibu na majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa mapato unafanyika kwa urahisi hata maeneo ya pembezoni.

Mfumo huu wa TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato tayari umeanza kutumika kwa baadhi ya mikoa na umeonesha ufanisi mkubwa, hivyo Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeamua kutumia mfumo huo katika ofisi zote za Warajis Wasaidizi wa Mikoa.