Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania( TCDC), Abdumajid Nsekela, amesema TCDC imedhamiria kuboresha mfumo wa Ushirika na kuwa wa kibiashara na kisasa zaidi.Amesema lengo ni kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta mbalimbali na kuongeza mchango wa Ushirika katika kupambana na umasikini pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

Nsekela amesema hayo leo tarehe 14/02/2023 wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salam. Pia Mwenyekiti amesema  Kamisheni inaweka nguvu katika uanzishwaji wa Mfumo wa kidijitali ili kuongeza ufanisi wa Vyama vya Ushirika na kuimarisha taasisi zinazohusika na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika.

"Tutaendelea kutoa elimu juu ya dhana ya Ushirika ili kuongeza ushiriki wa sekta mbalimbali, na kuharakisha mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika," amesema Nsekela. Aidha, Mwenyekiti wa Tume Nsekela amesema TCDC  kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Ushirika(TFC) wameandaa Mkutano maalumu wa Wadau wa Sekta ya Ushirika unaotarajiwa kufanyika Februari 27, 2023.

Kwa Upande wake Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt Benson Ndiege, amesema Sekta ya Ushirika imeboreshwa na kuongeza wigo wa Ushirika katika sekta mbalimbali na pia kuongezeka kwa mitaji katika vyama na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali hususani katika sekta ya Kilimo ambapo tozo za mazao 12 zinakusanywa kupitia Ushirika.

Dkt. ndiege amesema kuwa katika mwaka 2021/2022  Serikali ilipokea jumla ya Shilingi 15,144,077,319.16 zikiwa ni fedha za ushuru unaotokana na zao la Korosho uliolipwa na Vyama vya TANECU, MAMCU, RUNALI, LINDI MWAMBAO, TAMCU NA CORECU na shilingi 1,041,957,051.00 zimepokelewa na Mamlaka za Serikali  kama ushuru kutoka katika Vyama vya Ushirika KDCU NA KCU akupitia zao la Kahawa.