Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe, ametoa wito kwa kila Mdau anayehusika katika matumizi na usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kutimiza wajibu wake katika nafasi yake ili kupata masoko ya mazao ya wakulima  yenye ushindani.

Mhe. Kigahe ameyasema hayo Juni 28, 2023 wakati wa Siku ya Stakabadhi ya Ghala kwenye wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani iliyoanza Juni 26, 2023 na kilele cha Maadhimisho hayo kitakuwa Julai 01, 2023 katika Viwanja vya Nanenane Mjini Tabora.

Amesema matumizi ya Stakabadhi za Ghala yana umuhimu  katika kukuza sekta ya biashara na masoko ya bidhaa nchini. Hivyo, wadau wanaohusika na Mfumo huu wakiwemo wakulima, watendaji katika Vyama vya Ushirika, wasimamizi wa maghala kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Stakabadhi za Ghala ili kukuza ushindani wa soko kwa kuwapa wakulima bei nzuri yenye tija.

“Kama mnavyofahamu, Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unajumuisha wadau mbalimbali wakiwemo Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Waendesha Ghala, Mameneja Dhamana, Wakulima na Wazalishaji wa bidhaa nyingine, Taasisi za Fedha, Kampuni za Bima, Wakaguzi wa Ghala, Vyama vya Ushirika na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX). Ufanisi katika kufikia malengo ya Mfumo wa unategemea  utekelezaji wa wajibu wa kila mdau,” alisema Mhe Kigahe.