Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala umetajwa kuwa ni moja ya nyenzo ya kumsaidia mkulima kupata mauzo mazuri ya Wakulima. Hivyo kumuwezesha Mkulima kufaidika na Kilimo kupitia mfumo wa Ushirika. 

Hayo yamesemwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege leo Jumanne Mei 19,2020 wakati akiwa katika kikao na Maafisa Ushirika wa Mkoa wa Morogoro, kwenye ziara ya kikazi mkoani Morogoro.

Alieleza kuwa mfumo wa Stakabadhi ya Ghala ni kati ya hatua ya kuleta nguvu ya pamoja kupata manufaa zaidi na kusaidia upatikanaji wa masoko kwa rahisi na uhakika zaidi. Akisisitiza kuwa Maafisa Ushirika kuusimamia mfumo huu kama ambavyo Serikali ina azma ya kuinua Uchumi wa wanyonge kupitia mfumo wa Ushirika wa Stakabadhi ya Ghala.

“Ni jukumu letu kuusimamia Ushirika kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuhakikisha wakulima wananufaika na Kilimo kupitia Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala hususan hivi sasa tunapoelekea katika msimu wa mazao,” alisisitiza Mrajis 

Akupokea taarifa ya Ushirika ya Mkoa wa Morogoro Mrajis ameshauri mfumo wa Stakabadhi ya Ghala Mkoani hapo utaongeza tija ya Ushirika kutokana na kwamba mkoani hapo kuna maeneo mengi ya yanayofaa kwa mazao, pamoja na fursa nyingine za Ushirika. Aliongeza kuwa Maafisa Ushirika waendelee kuzingatia taratibu za usimamizi wa Ushirika kwa lengo la kupanua wigo wa Ushirika katika kuongeza uzalishaji na uendelezaji wa viwanda, ufugaji na madini katika maeneo yao ya kazi.

Akitoa taarifa ya Mkoa Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro Kenneth Shemdoe amesema mkoa huo una Jumla ya Vyama vya Ushirika 543, baada ya vyama 288 kufutwa katika katika Daftari la Vyama vya Ushirika, kati ya hivyo SACCOS NI 368, AMCOS ni 112 na Vyama vingine 71.