Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, tarehe 5 Agosti, 2022 amezindua jengo la Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha LULU SACCOS, Jijini Mbeya.Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Jengo hilo, Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge amewapongeza Wanaushirika wa LULU SACCOS kwa hatua hii kubwa ya Chama cha Ushirika kumiliki jengo lake.

 Mhe. Spika amehimiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kuendelea kuvisimamia na kuvishauri ipasavyo Vyama vinavyofanya maendeleo kama ya LULU SACCOS.Aidha, Mhe. Spika amewataka LULU SACCOS Kuendelea kuwa Chama bora cha Ushirika wa Akiba na Mikopo kwa mkoa wa Mbeya na Taifa kwa ujumla.

LULU SACCOS inatarajiwa kutoa Gawio la Hisa za umiliki wa jengo hilo ili kuwapa hamasa  wanachama wake na kuchangia katika pato la taifa kupitia kodi ya zuio itakayotokana na Malipo ya Pango la ofisi.

Vilevile, Mapato kutokana na jengo hilo yataimarisha zaidi mtaji wa ndani ili kutokuwa wategemezi katika kuendesha shughuli za Chama na kuimarisha utolewaji wa  huduma zote  kwa wanachama na jamii inayowazunguka na kuziboresha ziwe za kisasa zaidi.

Akizungumza katika uzinduzi wa jengo hilo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa LULU SACCOS  na Vyama vyote vya Ushirika vinavyoshiriki kwenye kujiletea Maendeleo..