Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege,  amevitaka Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), kuandaa na kuwasilisha taarifa za utendaji na uendeshaji kwa Wasimamizi ili waweze kufanya tathmini na kutoa maoni na ushauri kwa vyama husika. SACCOS zenye Leseni Daraja B zinatakiwa kuwasilisha kila Mwezi na SACCOS zenye Leseni Daraja A zinatakiwa kuwasilisha kila baada ya miezi mitatu.

Mrajis wa vyama vya Ushirika alikuwa akifungua Kikao Kazi cha Mameneja wa SACCOS na Wadau Kuhusu Usimamizi na Uendeshaji wa Shughuli za SACCOS zilizopewa Leseni, ambacho kinafanyika Jijini Dodoma kwa siku mbili  kuanzia  tarehe 8 -9Machi, 2022.

“Mnatakiwa kuhakikisha mnatumia format iliyoandaliwa na TCDC badala ya kuwasilisha taarifa husika kwa kutumia format zenu zisizoendana na format iliyotolewa na ofisi na kusababisha changamoto wakati wa kufanya tathmini,” amesema Dkt. Ndiege.

Kila Mtendaji anayehusika kujaza na kuwasilisha taarifa hizo ametakiwa kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi na watakaoshindwa kuandaa na kutuma taarifa hizo kwa wakati, watatozwa faini ambazo watazilipa kutoka kwenye mshahara wake na si kutoka kwenye fedha za chama husika.

 

Dkt. Ndige amezitaka kila SACCOS zinapitisha na kuidhinisha bajeti yake kupitia Ofisi za Warajis Wasaidizi au Makao Makuu kutegemeana na ukubwa wa biashara husika, kufanya mikutano kwa mujibu wa Sheria, kushughulikia malalamiko ya wanachama kwa wakati pamoja na kuhakikisha zinatekeleza masharti ya Leseni za Vyama husika.

 

Kila SACCOS zimetakiwa kuhakikisha zinafanyia kazi Hoja za Ukaguzi wa Nje kwa lengo la kuondoa Hati Chafu. Amesema SACCOS zitakazoendelea kupata Hati Chafu, Watendaji wake (Meneja) watapaswa kuchukuliwa hatua ikiwemo kuondolewa kwenye nafasi yake kwa mujibu wa Kanuni ya 85(1)(g) ya Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha za Mwaka 2019 kutokana na kutokidhi sifa na vigezo vya kuendelea kuwa Meneja wa SACCOS.

Aidha, Mrajis amezitaka SACCOS kutumia Mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya kurahisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi kwenye vyama. Amsema anafahamu kuna baadhi ya mifumo ina changamoto ya ufanisi kwenye utendaji lakini isiwe sababu ya kushindwa kutumia mifumo ya TEHAMA kwenye SACCOS.

“Iwapo patakuwa na tatizo lolote linalohusiana na watoa huduma wa Tehama ambao ofisi yangu imewapatia vibali, mnapaswa kuniandikia barua ikielezea tatizo husika ili ofisi iweze kushughulikia na kuchukua hatua pale itakaposhindikana kutatuliwa kwa tatizo husika,” amesema Dkt. Ndiege.

Mrajis amewataka Watoa huduma za TEHAMA katika Vyama vya Ushirika kuhakikisha wanaweka fomu zote 11 zilizoandaliwa na TCDC kwenye mfumo wao ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa ili kupunguza changamoto kwa SACCOS zenye mifumo kuandaa taarifa husika bila kutumia mifumo. Mifumo hiyo itaunganishwa (intergrated) na Mfumo wa Usimamizi wa TCDC unaoandaliwa.

SACCOS zimetakiwa kuendelea kubuni bidhaa na huduma ambazo zinaweza kuwavutia wananchi wengi kujiunga kwenye SACCOS na kuendana na mahitaji ya soko la fedha nchini. SACCOS nyingi zimekuwa zikiendelea kutoa huduma kwa mazoea na hivyo kushindwa kutafuta vyanzo mbadala vya fedha na kusababisha kuendelea kutoza riba kubwa na kwenda kinyume na lengo la kuanzishwa kwake