Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewataka viongozi na Wanaushirika kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu za Ushirika katika uendeshaji wa vyama  ili kujenga Ushirika Imara wenye nguvu utakaoleta chachu na kuongeza malighafi za viwanda na uzalishaji wa bidhaa.

Ameyasema hayo wakati  akifunga Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mei 24, 2024 lililoanza Mei 23, 2024 katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma likiwa na Kauli Mbiu “Ushirika hujenga kesho iliyo bora kwa Wote.”

Mhe. Senyamule amesema Vyama vya Ushirika vinapozalisha malighafi za kutosha kutokana na mazao ya kilimo, uvuvi, ufugaji, nyuki na madini vinasaidia Serikali kufika Mpango wa Maendeleo endelevu ya Uchumi wa Viwanda kwaajili ya Maendeleo ya Wananchi.

Katika Jukwaa hilo, Kaimu Naibu Mrajis (Uhamasishaji), Consolata Kiluma, amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaendelea kuvisimamia Vyama vya Ushirika ili viweze kujiendesha kisasa kwa kutumia mifumo ya kidijitali ikiwemo Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) ili kuongeza uwazi na upatikanaji wa taarifa za vyama kwa usahihi na kuleta tija ya uzalishaji.

Aidha, taarifa ya Wanaushirika  iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo,  Andrew Ntomola, imeeleza Vyama vyenye Hati Safi mkoani Dodoma vimeongezeka kutoka 7 hadi 12, vyama vyenye hati zenye shaka vimepungua kutoka 40 hadi 26 na vyama vyenye hati mbaya vimepungua kutoka 66 mwaka 2022 hadi 6 mwaka 2023.            

Pamoja na mambo mengine, Baadhi ya Vyama vya Ushirika washiriki wa Jukwaa hilo vimepata tuzo  kutokana na vigezo vya ubunifu wa Bidhaa, huduma Bora, ukuaji wa kasi wa mitaji endelevu, uwasilishaji wa makisio ya Vyama kwa wakati, matumizi ya Mifumo pamoja na ukuaji wa Akiba na Amana.