Tume ya Maendeleo ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imeagizwa kuhakisha kuwa Vyama vya Ushirika vinajiendesha kibiashara kwa kutumia misingi thabiti ya Ushirika pamoja na matumizi mazuri ya rasilimali zilizopo katika Sekta ya Ushirika ili kutengeneza faida na kuwanufaisha wanaushirika na hatimaye kuongeza Pato la Taifa.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, jana Mei 7, 2020 alipozungumza na Makamishna wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Menejimenti ya TCDC Jijini Dodoma.

Naibu Waziri amesema Ushirika ni Sekta muhimu kwa uchumi wa Taifa hivyo ikisimamiwa vyema itaweza kutoa mchango mkubwa kwa wananchi. Alisema Ushirika usiendelee kubaki kama huduma pekee bali uendeshwe kwa kufuata taratibu za kibiashara kama vile kuwa na mifumo thabiti ya ufuatiliaji wa mauzo, makusanyo ya mazao na malipo ya wakulima.

Aidha, Mhe. Bashe ameitaka TCDC kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinaajiri Wataalam mbalimbali ili waweze kusaidia katika uendeshaji wa vyama hivyo kibiashara na kuinua uchumi wa wanaushirika.

 “Ni lazima sasa tufikirie kibiashara zaidi, kwa kusimamia Vyama vya Ushirika vizalishe kwa faida, tuweke mifumo unganishi itakayoweza kuonesha kazi na shughuli za kila siku za Chama. Hii itatusaidia kubaini changamoto na kuzitatua na hatimaye kuondokana na ubadhilifu unaojitokeza mara kwa mara katika Vyama vya Ushirika,” alisema Mhe. Bashe

Naibu Waziri ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kutengeneza mifumo ya kisasa itakayotumika kupata taarifa pamoja na kutunza kumbukumbu za Vyama kuanzia Vyama vya Msingi na Vyama Vikuu ili Mwanaushirika aweze kupata malipo yake sahihi.

 Aidha, Mhe. Bashe amevishauri Vyama vya Ushirika kusajili makampuni ya kibiashara ambayo yatafanya kazi kwa mwelekeo wa kibiashara zaidi kwa maslahi ya wanachama. Makampuni hayo yarahisisha kuingia makubaliano ya kibiashara, kutambua na kuzitumia fursa mbalimbali za uwekezaji pamoja na utafutaji wa masoko kwa niaba ya Vyama vya Ushirika na Wanachama wa vyama hivyo.

Akiongea katika kikao hicho kwa niaba ya Makamishna, Kamishna Robert Busumabu alimpongeza Naibu Waziri kwa kuwa miongoni mwa viongozi wa mstari wa mbele katika kusimamia na kufuatilia maendeleo ya Ushirika nchini. Alisema Tume ipo tayari kwa utekelezaji wa maagizo na ushauri muhimu aliotoa na kuahidi kwamba taratibu za utekelezaji zitaanza mara moja.