Mkuu wa Mkoa wa Lindi na Kamishina wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Mhe. Zainab Telack amekabidhi gari kwa Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Lindi. Gari Hilo limetolewa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) limekabidhiwa leo tarehe 18/05/2023 wakati wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa wa Lindi lililofanyika Mjini Lindi likiwa na kauli mbinu "Ushirika ni Biashara". Kwenye jukwaa hilo Mkuu wa Mkoa,ametoa rai kwa wana Lindi wanaojishugulisha na masuala ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji kujiunga na Vyama vya Ushirika ili waweze kuuza kwa pamoja kwenye soko.
“Hata Kama mnafanya shughuli za mtu mmoja mmoja kwenye mauzo ni muhimu muuze pamoja kwani Ushirika unapandisha hadhi ya mazao na bidhaa na Ushirika ni mwamvuli wa wakulima na ndiyo mtetezi wa wanyonge,” amesema Mhe. Telack. Mkuu wa Mkoa amesema uaminifu na uadilifu ndiyo nguzo ya Ushirika imara hivyo viongozi wakiingia kwenye ushirika waende wakafanye kazi kwa uadilifu na waache mawazo ya kuwa kwenye Ushirika ndiyo kwa kupatia fedha bila utaratibu.
Kwa upande wake Naibu Mrajis - Uhamasishaji, Consolata Kiluma, amevitaka Vyama vya Ushirika Mkoani Lindi kushirikiana na Maafisa Ushirika na ofisi ya Mrajis Mkoa kujibu hoja za wakulima kwa wakati. Pia Naibu Mrajis amesema, Vyama vya Ushirika Mkoa wa Lindi vimefanikiwa kusajili vyama ila idadi ya wakulima na wanachama wamewasajili wachache hivyo wamalizie kusajili wakulima wao wote wanaowahudumia.
Aidha, Naibu Mrajis ametoa wito kwa wanaushirika wote kuhudhuria kwa wingi Siku ya Ushirika Duniani inayotegemewa kufanyika mkoani Tabora kuanzia tarehe 26/06/2023 hadi 01/07/2023.“Siku ya Ushirika kitaifa ni ya wanaushirika wote na ili ifanikiwe wanachama inabidi mtoe michango na mhudhurie kwa wingi tuendele kuhamasishana tunavyorudi kwani kila Mkoa utakuwa na mabanda yake na tunategemea Ushiriki na michango yenu ili tufanimishe siku hiyo,”amesema Consolata.