Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahya Nawanda, amesema Mkoa wa Simiyu umedhamiria kuanzisha viwanda kwa ajili ya kuongeza ajira na kukuza uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.Dkt. ameyasema hayo alipokuwa akizindua Jukwaa la tatu la Ushirika Mkoa wa Simiyu tarehe 27 Aprili, 2023 Mjini Bariadi.Dkt. Nawanda amesema viwanda vitakavyoanzishwa vitatumia mali ghafi zitazokuwa zinazapatikana kupitia Vyama vya Ushirika na Wakulima wa Mkoa huo na mikoa ya jirani.
Jukwaa la Ushirika mkoani Simiyu lililozinduliwa leo na kuhudhuriwa na Makamu Mwenyekiti Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Irene Madeje na Naibu Mrajis - Uhamasishaji Consolata Kiluma, Mrajis Msaidizi Mkoa wa Simiyu, Godfrey Mpepo na Wadau wa Ushirika pamoja na Viongozi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu linalenga kuweka Mkakati wa Pamoja wa kuimarisha Vyama vya Ushirika mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amesema mkakati ulioko kwa sasa ni kujenga Viwanda Bariadi Dc na Bariadi Tc ambavyo viwanda hivyo vitaweza kuzalisha ajira 800 - 900 katika viwanda hivyo, na katika Wilaya ya Busega kutajengwa kiwanda kikubwa cha Sukari ambacho kitazalisha ajira elfu 20.Dkt. Nawanda amesema Mkoa wa Simiyu unalenga kuongeza uzalishaji wa zao la Pamba kufikia tani laki tatu (300,000) ambapo asilimia 60 ya Pamba Hai Nchini inazalishwa katika mkoa wa Simiyu.
Akizungumza katika uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika, Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Irene Madeje amewasisitiza Wanaushirika kutumia ipasavyo Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) kuweza kusaidia katika kusimamia mali za Ushirika.
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ushirika amevitaka Vyama vya Ushirika kuhama kutoka katika matumizi ya pesa taslimu na kuhamia kwenye kutumia Pesa Mtandao (moneyless).