Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dkt. Rashidi Chuwachuwa, amewataka Warajis Wasaidizi wa Mikoa, Maafisa Ushirika, Wenyeviti na Mameneja wa Vyama vya Upili kutumia vizuri mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika ili yaweze kuwasaidia katika utendaji wa majukumu yao ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ushirika.

Dkt. Chuachua ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) kwa mikoa ya Mbeya, Iringa, Niombe, Rukwa na Songwe yaliyoanza leo tarehe 15/12/2022 Jijini Mbeya.

"Mafunzo haya yatasaidia sana katika suala zima la uwajibikaji na uwazi katika vyama vya Ushirika kwani wakulima wanategemea Vyama vya Ushirika katika kutatua changamoto walizonazo; hivyo mtumie mfumo huu katika kutatua changamoto mbalimbali za wakulima,"alisema Dkt.Chuachua.

Ameongeza kuwa Ushirika ni nguzo kuu katika utatuzi wa changamoto za wakulima maana kama hakuna wakulima hakuna Ushirika, hivyo wasimamizi na watendaji wawe msaada katika kuwapa taarifa sahihi na kwa wakati.

Akimwakilisha Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Valency Karunde amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kama nguzo kuu katika kurahisisha utoaji wa taarifa zenye usahihi na kwa wakati ili kupunguza  ubadhirifu katika Vyama.

"Mfumo huu wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika utatusaidia kupata taarifa kutoka kwenye vyama na kutoka kwa wadau mbalimbali wa Ushirika kwa wakati na Serikali inategemea kupata taarifa hizo kwa wakati na kwa usahihi," alisema Karunde, ambaye ni Mhasibu Mkuu wa TCDC.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Hermes Rulagirwa amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo umuhimu wa Mfumo huu wa MUVU kuwa wayazingatie maelekezo yanayotolewa ili kuwa rahisi kuviboresha Vyama vya Ushirika katika ngazi zote. 

Mafunzo haya ya MUVU tayari yamefanyika katika mikoa 23 ya Tanzania Bara na yanategemea kukamilishwa katika mikoa yote; na Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imekabidhi kompyuta mpakatato kwa Warajis wa Mikoa husika ili kuwasaidia katika  utoaji wa taarifa za Vyama vya Ushirika wa mfumo wa MUVU.