Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhakikisha Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) unaendana na mifumo ya Vyama vya Ushirika ili iwe rahisi kwa Tume kujua jinsi Vyama hivyo vya Ushirika vinavyofanya kazi yake kila siku.

Mfumo huo ukiunganishwa na Mifumo ya Vyama vya Ushirika utasaidia vyama vingi kutokufa kwasababu Tume itakuwa inajua Muundo wa uendeshaji wa shughuli za kila siku za Vyama hivyo na mwenendo wake kwa ujumla.

Waziri Mhe. Bashe ameeleza hayo leo tarehe 17/10/2022 wakati akifungua Wiki ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo yanayofanyika Jijini Mwanza kwenye viwanja vya Furahisha.Pia ameagiza Sera ya Usimamizi na uendeshaji wa Benki za Ushirika na Taasisi nyingine za kifedha ziboreshwe ili ziweze kuendana na uhalisia na mahitaji ya Wanaushirika na mazingira yao ya uzalishaji.

"Benki hiyo ya Taifa ya Ushirika ikifanikiwa kuanzishwa  kilio cha wanaushirika kukosa mitaji itakuwa imekwisha kwasababu watakuwa na chanzo cha kupata mikopo yenye riba nafuu; cha msingi nunueni hisa benki yenu izidi kukua," amesema Mhe. Bashe.

Vile vile ameagiza Maadhimisho ya Kitaifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo kwa mwaka 2023 (ICUD 2023) kufanyika tena Mkoani Mwanza ili kusaidia kukua kwa uchumi wa eneo husika na Vyama pia.

Kwa upande wake Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirikia Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amesema Tume imeendelea kutumia Mifumo ya TEHAMA katika Usimamizi wa Vyama vya Ushirika.

 "Tunaendelea kufanya kazi kwa kufuata taratibu na miongozo ambayo pia inatutaka kusimamia mali za Ushirika kupitia Miongozo iliyoandaliwa kwa ajili ya kuboresha Usimamizi wa Vyama hivyo. Miongozo hiyo itasaidia kuonesha mwelekeo kwa Warajis wa Mikoa na Maafisa Ushirika wa Wilaya," amesema Dkt. Ndiege.