Mfumo wa usimamizi wa Vyama vya Ushirika ulioanzishwa na Serikali kupitia Tume Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) utaenda kuimarisha vyama vya ushirika.
Mwakilishi wa Katibu Tawala ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam, Saloni Nyika amesema Mfumo wa usimamizi wa vyama vya ushirika utaenda kuimarisha vyama vya ushirika na kufanya utambuzi wa wanachama. Amesema hayo leo tarehe 09/11/2022 wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika yaliyofanyika ukumbi wa Ngome Holdings, Jijini Dar es Salaam.
Bwana Nyaki amesema sasa ni wakati sahihi kwa vyama vyote na taasisi za serikali kuhamia kwenye mifumo ya kidigitali na kuachana na mambo ya makaratasi. “Tume inaenda na wakati na inazingatia maelekezo ya Serikali kwa Ofisi zote za Serikali kutumia mifumo katika utendaji kazi wao; nawapongeza Tume kwa kwenda na kasi ya Serikali yetu,” amesema Nyaki
Aidha, alisema Mfumo ulioanzishwa na TCDC utarahisisha utunzaji kumbumbuku wa vyama vyote pamoja na utunzaji na utambuzi kwa mali na madeni ya vyama na itakuwa rahisi kutoa taarifa zinazohitajika. Wakati huo huo Mwakilishi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika ambaye pia ni Mhasibu Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Valency Karunde, amesema Vyama kujiunga na kutumia mfumo huu wa Usimamizi wa Vyama vya uuhirika si suala la hiari.
Ameeleza kuwa kila chama kinatakiwa kujiunga na kujisalljili na kupata cheti kipya mpaka desemba na chama ambacho hakijajisajili kitakuwa hakitaki kuendelea kuwa chama cha Ushirika ambacho kinasimamiwa na Tume.
"Msingi mkubwa ni uwazi na uwazi ndiyo mawasiliano, ukiingiza taarifa inayosoma ndiyo sahihi na mtu huwezi kufuta; kwa daftari ni rahisi mtu kughushi," amesema Karunde. Aliendelea kuwasisitiza Viongozi wa Vyama vya Ushirika kufanya kazi kwa uwazi na kutumia mifumo ili kuimarisha uwazi huo na huu ni wakati sahihi wa mfumo kuanza kufanya kazi.