Makabidhiano ya mali za uliokuwa ushirika wa Mara Cooperative Union (1984) Ltd kwa Vyama Vikuu vya Ushirika vya PAMBA MARA na  WAKULIMA WA MARA  yamefanyika tarehe 12 Desemba, 2022 katika Kiwanda cha Kuchambua Pamba na Mafuta ya Pamba cha Mgango  katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gambaless Timotheo, ameeleza kuwa urejeshaji wa mali hizo za ushirika utasaidia kuchochea ukuaji wa kilimo cha mazao ya Pamba na Kahawa katika mkoa wa Mara.

"Ni matumaini yangu mtakuja na mkakati madhubuti wa kuendeleza viwanda hivi na kuzitunza mali za ushirika mlizokabidhiwa leo kwa manufaa ya wanaushirika wote wa Mkoa wa Mara," alisema Timotheo.  

Bwana Timotheo ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Mfilisi kwa kusimamia zoezi hilo vizuri na kuhakikisha Vyama hivyo vinapata mali zao zikiwa salama na makabidhiano yamefanyika kwa amani. 

Kwa upande wake, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, ameeleza kuwa mgawanyo wa mali na madeni kwa Vyama hivyo umetegemea zaidi mazao wanayoshughulika nayo. 

Ameeleza kuwa katika mgawanyo huo, WAMACU wanapata Kiwanda cha Kahawa cha Tarime, ardhi ya kiwanda hicho na asilimia 19.25 ya deni lote lililobakia wakati PMCU inapata viwanda vya Pamba vya Mugango (Musoma), Kibara  na Ushashi (Bunda) pamoja na ardhi ya viwanda hivyo na mali zilizomo na madeni asilimia 80.75.

Mali zilizokabidhiwa ni pamoja na viwanda vinne vya mazao vyenye thamani ya Shilingi bilioni 5.2 na madeni ya Shilingi bilioni 1.8.