Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema Serikali imeendelea na hatua mbalimbali za mageuzi katika Sekta ya Ushirika ili kuimarisha Uchumi na kuleta Maendeleo kwa Wananchi wengi nchini.
Waziri Mkuu amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Ushirika lililofanyika leo Aprili 27, 2025 kuelekea Uzinduzi wa Benki ya Ushirika utakaofanyika kesho Aprili 28,2025 Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amebainisha baadhi ya hatua zilizofanyika katika kuimarisha Ushirika ili kuongeza kasi ya kukuza Uchumi ni pamoja na kuboresha Mifumo ya Usimamizi ya Ushirika, kuimarisha masoko ya mazao kupitia Stakabadhi za Ghala, upatikanaji wa Pembejeo pamoja na uboreshaji wa huduma za Fedha ikiwemo kuanzisha Benki ya Ushirika.
Aidha, ametoa wito kwa Wadau wa Maendeleo na Taasisi za kifedha kushirikiana na Benki ya Ushirika ili kuwa sehemu ya mageuzi ya Ushirika yatakayokuwa chachu ya maendeleo ya Wanaushirika na Wananchi wengi kupitia kilimo, uvuvi, ufugaji na Sekta nyingine za kiuchumi.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema Benkiya Ushirika inamilikiwa na Wanaushirika kwa asilimia 51 jambo ambalo litachangia itaongeza tija katika Ushirika kwa kuwasaidia Wanaushirika kupata Mikopo ya kuendesha shughuli zao kiuchumi kwa kuelewa mahitaji maalum ya Wakulima na Wanaushirika wengine.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Abdulmajid Nsekela amebainisha kuwa uanzishaji wa Benki ya Ushirika ni utekelezaji wa Vipaumbele vya Tume, ambayo itasaidia kuhudumia Sekta mbalimbali na kuleta ujumuishi wa Kifedha na kufikia Wananchi wengi.
Aidha, shughuli nyingine zilizofanyika katika Kongamano hilo ni pamoja na uzinduzi wa Taarifa ya Kilimo ya Mwaka 2022/23- 2023/24, Utiaji saini wa hati za Makubaliano ya Mashirikiano ya Taaasisi mbalimbali na Benki ya Ushirika, Utoaji wa Tuzo kwa michango na Uwekezaji wa kuhamasisha uanzishaji wa Benki ya Ushirika.
Benki ya Ushirika inatarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Jijini Dodoma.