Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC), Bw. Tito Haule, amewapongeza Watumishi wa Tume hiyo kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Ushirika nchini katika kipindi cha miaka miwili na nusu akiwa kiongozi mkuu wa taasisi hiyo.

‘Mafanikio mbalimbali yamepatikana katika vyama vya ushirika nchini, na mafanikio hayo siyo ya mtu mmoja, ni yetu sote. Kila mmoja katika nafasi yake amechangia kwa kiasi kikubwa katika mabadiliko yanayoonekana sasa kwenye vyama vya ushirika,’ amesema Mrajis.

Bwana Haule alikuwa akizungumza na Watumishi wa Tume Makao Makuu na Warajis Wasaidizi wa Mikoa kwenye Mkutano alioutisha ili kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Tume katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita tangu alipoanza kuiongoza Tume ya Maendeleo ya Ushirika.

Mrajis amewataka Wafanyakazi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kote nchini kuendelea kujituma katika utendaji kazi wao ili kuongeza ufanisi katika kazi zao kwenye Sekta ya Ushirika na kumsaidia mwananchi wa kipato cha chini kujikomboa kiuchumi.