KONGAMANO LA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA LAFANYIKA KWA MAFANIKIO

Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe leo tarehe 30 Juni, 2022 amefungua Kongamano la Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, lililofanyika Mjini Tabora kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) mwaka 2022.

Mhe. Naibu Waziri amewapongeza Wanaushirika kwa kuendelea kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika kuuza kwa pamoja kupitia minada na utafutaji masoko ili kupata bei nzuri za mazao yao.  

Mhe. Kigahe ameyataja Mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni pamoja na ongezeko la bei za mazao, mapato ya mkulima na Mapato ya Serikali kwa wastani wa asilimia 200; na ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka. 

Mafanikio mengine ni Mfumo kuwa kichocheo cha Ubora wa mazao yanayofikishwa sokoni; upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao; na kukuza  huduma za fedha vijijini na kufanikisha Uanzishwaji wa Soko la Bidhaa Tanzania.

Mfano wa manufaa ya bei ni zao la Choroko kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala imeongezeka kwa asilimia 25, zao la Kakao imeongezeka kwa asilimia 250 na bei ya zao la Korosho imeongezeka kwa asilimia 168 ikilinganishwa na bei wakati wa Mfumo holela wa mauzo ya mazao hayo.

Akizungumza katika Kongamano hilo Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amewataka Wanaushirika kuimarisha matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kuwawezesha Wanaushirika Kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na kukuza kipato chao.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya   Stakabadhi za Ghala, Asangye Bangu, amesema Bodi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007/2008 katika zao la Korosho imeendelea kupanuka katika mazao mbalimbali ikiwemo Ufuta, Kakao, Kahawa, nafaka na mazao jamii ya Kunde.

Bangu amesema hadi kufikia msimu wa 2021/2022, Bodi imesimamia ukusanyaji kupitia Mfumo zaidi ya Kilogramu billioni 2.3, na kuleta utulivu wa mtiririko wa Bidhaa kutoka shambani hadi sokoni ikilinganishwa na mazao yanayouzwa kupitia mifumo isiyo Rasmi.