Kikao kazi cha Mafunzo kwa watekelezaji wa Sheria ya Ushirika  kutoka Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote nchini kimefunguliwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, Jijini Dodoma na kilichofanyika  kuanzia  tarehe 9 - 11 Machi, 2022.

Kikao kazi hicho kimeandaliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kimenafanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Conventional Centre na kinawahusisha Wanasheria Kutoka Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote Nchini.

Mafunzo hayo yanahusu namna bora ya kutekelezaji Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya Mwaka 2013 na Miongozo mbalimbali inayosimamia Sekta ya Ushirika ili kuwawezesha Wataalam hao wa Sheria kutoa Ushauri kwa Viongozi mbalimbali katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na Viongozi na Wanachama wa Vyama vya Ushirika.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mafunzo hayo, Dkt. Ndiege amesema nafasi ya Wanasheria wa Mikoa katika Usimamizi na Utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Ushirika ni muhimu ili kuviwezesha vyama vya Ushirika viweze kupata ushauri wa karibu wa kisheria jinsi ya kutatua changamoto zinazojitokeza katika Uendeshaji wa Vyama; badala ya kusubiri Wanasheria wa TCDC kutoka Dodoma.

Mrajis amewaasa Wanasheria hao wa Mikoa kuvisaidia Vyama vya Ushirika katika kutatua migogoro mbalimbali inayojitokeza katika Usimamizi na Uendeshaji wa Vyama hivyo, na amewataka kutumia ipasavyo Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya Mwaka 2013, Kanuni na Miongozo ya Ushirika kwenye Ushauri watakaoutoa.