Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imeshiriki katika Uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya kuratibu harambee ya ujenzi wa eneo la Mradi wa Kiwanda cha Wanawake Tanzania kilichoratibiwa 'Madirisha Women Cooperative Society' kilichofanyika katika wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani.

Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu Harambee hiyo, Waziri Mstaafu, Mama Anna Abdallah, ametoa pongezi kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa namna wanavyosimamia na kuhamasisha Maendeleo ya Vyama vya Ushirika nchini.Aidha, Kupitia Ushirika wanawake wataweza kujikwamua kiuchumi na kijamii kama wataamua kuunganisha nguvu zao kiuchumi kupitia Ushirika na kusimamia malengo yao.

Mama Anna Abdallah, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi ametoa pongezi hizo  leo tarehe 19/09/2022 wakati wa uzinduzi wa eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza washiriki kuwa Ushirika ni kama dawa ukijiunga basi unakuwa umepata tiba ya ugonjwa wako kwani husimamiwa kwa mujibu wa Sheria, taratibu na miongozo mingine.

"Chombo chochote kinachofuata Sheria katika kufanya kazi zake ni lazima kifikie malengo yake, nawashauri wanawake wote nchini kujiunga katika Vyama vya Ushirika ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao na kufikia malengo kwa wakati," alisema Mama Anna Abdallah.

Aidha, aliendelea kusisitiza kuwa Ushirika wa Madirisha utafanikiwa zaidi kama wanachama watadumisha  upendo na uzalendo katika utendaji kazi zao kwa sababu rafiki wa mwanamke ni mwanamke. "Pendaneni na aminianeni, hii ni nguzo ya mafanikio kama mkiisimamia na ninawaamini wanaushirika wa Madirisha mtafanikiwa kujenga kiwanda na mkauza bidhaa hizo ndani na nje ya nchi." 

Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, amesema Ushirika wa Madirisha ni wa kuigwa kwani kina mama hawa wameweza kuunda Ushirika na kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zinaendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali.

"Ushirika huu ni wakipeeke sana na sasa ni wakati wa wanawake na vijana kuwa na maono mapana na makubwa kama haya ya Madirisha na kuacha kufikiri biashara ndogo ndogo."Vilevile, alisema Wakinamama wengi wanafanya biashara nyingi ila hazikui hivyo sasa ni muda muafaka kina mama kuingia katika uzalishaji na uuzaji kwa mfumo mkubwa kupitia Ushirika.

Hata hivyo, Mrajis amesema Tume sasa ina malengo ya Kuongeza Ushiriki wa vijana na kina mama katika kuunda ushirika mbalimbali ambao Tume utaisimamia kwa kufuata utaratibu.

Mwenyekiti wa 'Madirisha Women Cooperative Society' aliwaeleza washiriki wa harambee kuwa Ushirika wa Madirisha wa Wanawake ulianzishwa mwaka 2020 ambapo Ushirika huo unajishughulisha na viwanda vya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama vile utengenezaji wa Mlonge, Ufugaji wa Samaki, sabuni, Maziwa, Batiki, Usafi na Mazingira ,Nafaka na Lishe, Mafuta na Gesi, Mafuta ya Nazi, Asali, Viungo, Shanga na Urembo.