Benki ya Ushirika  Kilimanjaro (KCBL)  Alhamis, Februari 03, 2022 imeadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa  kwake, ambapo Benki hiyo imefanikiwa pamoja na mambo mengine kutoa mikopo kwa Wakulima, Vijana, pamoja na Wafanyabiashara ndogondogo.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, aliyewakilishwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Andrew Masawe

 

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, katika hotuba iliyosomwa kwaniaba yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Andrew Masawe, ameitaka  Benki ya KCBL kuendelea  kutoa huduma za mikopo kwa Wakulima, Vijana, Pamoja na Wafanyabiashara ndogondogo; na mikopo hiyo itolewe  kwa riba nafuu.

 

Aidha, Benki ya CRDB imetakiwa kuendelea kuisimamia Benki hii ya Ushirika KCBL ili kuyatekeleza yote waliyoyapanga na kukubaliana.

 

Waziri Bashe ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika  kuendelea kuisimamia benki hii ya Ushirika ili iweze kufuata Misingi, Kanuni na Sheria za Ushirika katika uendeshaji wake. 

Akizungumza katika Maadhimisho hayo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, 

amesema TCDC itaendelea kusimamia Benki ya KCBL na kuendelea kuhamasisha Vyama vya Ushirika kununua Hisa katika Benki hiyo. 

"Imetuchukua miaka miwili kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhamasisha Vyama kulielewa wazo hili la kuwa na Benki ya Ushirika, haikuwa rahisi," alisema Mrajis.