Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika kutawawezesha Wanaushirika  na Wanaanchi kwa ujumla kumiliki Uchumi wao na kupata huduma kwa urahisi ambapo watapata mitaji itakayotolewa kwa riba ndogo ukilinganisha na Taasisi nyingine za kifedha.

Mrajis ameyasema hayo leo Aprili 22, 2022 akiwa Mgeni Rasmi kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, katika Mdahalo wa Kitaifa wa Uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika kuhusu Uchambuzi wa Fursa na Changamoto kutokana na kuanzishwa kwa benki hiyo. Mdahalo umefanyika mjini Moshi kwenye Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) na kuhudhuriwa na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Ushirika na Taasisi za Fedha ikiwemo benki.

Dkt. Ndiege amesema Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, imechukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuhakisha kuwa Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) inaendelea kuwepo na kuwezeha kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika.

Hatua zilizochukuliwa ni Pamoja na Kuhamasisha SACCOS zote zilizokuwa zimewekeza kwenye Benki ya KCBL kukubali kufanya mabadiliko na kuruhusu akiba zilizokuwa zimekezwa ziwe sehemu ya hisa za Benki kwa lengo la kuongeza Mtaji wa Benki; na kuhamasisha wanaushirika kuwekeza kwenye Benki hii ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa TFC kuhamisha Fedha zilizokuwa zimekusanywa zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni mia nne kuingizwa KCBL kwa lengo la kuiongozea uwezo wa kifedha na kupata Mtaji unaotakiwa.

Aidha, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeendelea kufanya Usimamizi na kuutoa maelekezo kwa KCBL ikiwemo kufanya tathmini ya Bajeti ya KCBL, kutoa Ushauri na kuidhinisha bajeti hiyo ili kuendana na mahitaji ya soko la Fedha.

Mdahalo huo ulioandaliwa na Benki ya Ushirika Kilimajaro kwa kushirikiana  na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi  ulihusisha mada mbalimbali ikiwemo Mafanikio, Mikakati na Muundo wa Benki ya Taifa ya Ushirika Tanzania; Historia ya Ushirika na Falsafa ya Benki za Ushirika; Mazingira ya Kisheria na Kisera: Je, yanawezesha Uendeshaji wa Kisasa wa Benki ya Taifa ya Ushirika?; Nafasi ya Wadau mbalimbali katika Uanzihwaji na Uendelezaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika; Nafasi ya Benki ya Taifa ya Ushirika katika kutoa huduma jumuishi za kifedha; Benki ya Taifa ya Ushirika na Ushidani katika tasnia ya Biashara ya Kibenki; Uzoefu wa Uanzishwaji na uendeshaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika; na Uwekezaji na Masoko.

Viongozi wengine waliohudhuria katika Mdahalo huo ni Pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TFC, Charles Jishuli; Mwenyekiti wa Bodi ya KCBL, Dkt. Gervas Machimu; Makamu Mwenyekiti KCBL, Chiku Issa; Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Profesa Alfred Sife; Mtendaji Mkuu wa Benki ya Ushirika Kilimajaro, Godfrey Ng’urah; Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Maregesi Shaban; Mkurugenzi wa Mikopo –Benki ya CRDB, Xavery  Makwi; Mrajis Msaidizi Mkoa wa Kilimanjaro, Jacqueline Senzige; na Mrajis Msaidizi Mkoa wa Arusha, Grace Msambaji.