Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) inashiriki Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yaliyoanza rasmi tarehe 28 Juni, 2022 hadi 13 Julai, 2022.

Kupitia Maonesho hayo yanayoendelea ndani ya viwanja wa Mwl Julius K. Nyerere maarufu SABASABA, Tume imeandaa Kijiji cha Ushirika kwa ajili ya wadau wake ikiwemo Vyama vya Ushirika, Wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali kwa ajili ya kuonesha bidhaa na huduma mbalimbali wanazotoa, kufanya Biashara na kutangaza fursa za uwekezaji katika maeneo yao ya Uzalishaji.

Baadhi ya Vyama vya Ushirika vinavyoshiriki kwenye Maonesho hayo ni pamoja na  USHIRIKA WA VIWANDA VIDOGO VIDOGO DAR ES SALAAM (DASICO), WAT SACCOS, CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA RUNALI, WETCU LTD, CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA MKOA WA SHINYANGA (SHIRECU LTD), MADIRISHA WOMEN COOPERATIVE SOCIETY, CHAMA CHA USHIRIKA CHA MSINGI IGALE na CHAMA CHA USHIRIKA CHA MSINGI IYULA. 

Wengine wanaoshiriki pamoja na TCDC ni Wadau wanaofanya shughuli zao kupitia Ushirika na wajasiriamali wanaotokana na Vyama vya Ushirika.

Kupitia Maonesho hayo Vyama vya Ushirika vinatangaza bidhaa wanazozalisha, huduma wanazotoa na fursa za uwekezaji kwa wadau mbalimbali walioshiriki Maonesho hayo

Leo Jumatano Julai 06, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege ametembelea Maonesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea ndani ya viwanja vya Mwl Julius K. Nyerere na kuvisisitiza Vyama vya Ushirika vilivyoshiriki kuongeza wigo katika uzalishaji kutegemeana na mahitaji ya soko ikiwa ni pamoja na kutambua fursa zinazopatikana kwa ajili ya kukuza Uchumi wa Vyama na wanachama wake.

"Ni vyema kwa kipindi kijacho, Kijiji cha Ushirika kikawa na wadau wake muhimu ikiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara wanaotokana na Vyama vya Ushirika," alisema Dkt Ndige.