Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ameviagiza Vyama vya Ushirika nchini kuendeleza zoezi la la upandaji wa miti katika maeneo yao ikiwemo mashamba wanayoyamiliki na kuzingatia utekelezaji wa Msingi wa Saba wa Ushirika katika kuijali Jamii kwa kupanda miti katika Taasisi za Umma ikiwemo shule, hospitali na maeneo mengine ya huduma za kijamii.
Ameelekeza hayo leo tarehe 11/01/20203 wakati wa Uzinduzi wa Zoezi la upandaji Miti lililofanyika katika shule ya Msingi Uhuru Jijini Dodoma ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira.
Amesema Dkt. Ndiege Lengo la zoezi hilo kuhamasisha Vyama vya Ushirika na Wanaushirika kutunza mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yao ikiwa ni utekelezaji wa Msingi wa Saba wa Ushirika wa kujali Jamii. Aidha, Tume imaemua kuhimiza upandaji wa miti ili kuunga mkono maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuifanya nchi kuwa ya kijani na kutunza mazingira
"Kwa kuwa Zoezi hili ni endelevu, natoa wito kwa Waandishi wa Habari kuendelea kuelimisha na kuhamasisha Wanaushirika na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na pia walimu na wanafunzi hakikisha miti iliyopandwa inatunzwa na kukua vizuri kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo"
Kwa upande wake Msimamizi wa Misitu Leonard Biromo ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kuona umuhimu wa kuanzisha kampeni ya upandaji miti ambayo itafanyika katika maeneo yote yenye Ushirika.
Ameeleza suala la kupanda miti ni la kila mtu na wao Wakala wa Misitu wanaendelea kushirikiana na watu na Taasisi zote zinazoitaji kufanya zoezi kama linalofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika.
Naye Mtendaji katika Chama cha Ushirika Janet Karinga kutoka PPRA SACCOS amesema wao kama Vyama wamepokea maelekezo ya Mrajis na watayatekeleza ,kuyasimamia na kuyafanyia kazi kama ambavyo inatakiwa.