Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika -Udhibiti, Collins Nyakunga, ametoa wito kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika Nchini kuhakikisha  wanafuata na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu za Ushirika pamoja na Miongozo inayotolewa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) ili kuhakikisha Vyama vinajiendesha kwa kuwanufaisha Wanachama na kuwa na misingi bora ya utendaji.  

Wito huo umetolewa leo Februari 22, 2024 na Naibu Mrajis akifunga Jukwaa la Pili la Viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) lililohusisha Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi wa Vyama vya SACCOS Jijini Arusha katika Jukwaa lililoratibiwa na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT - 1992) kuanzia Februari 20, 2024. 

Aidha, Naibu Mrajis amewataka Viongozi hao kuendelea  kukamilisha usajili wa Vyama katika Mfumo wa kidigitali wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) ili kuimarisha na kuendeleza Ushirika wa Kifedha katika hatua za kuimarisha utendaji wa SACCOS.

Pia amewataka viongozi hao  kuisaidia jamii na kurudisha manufaa katika jamii  kwa mujibu wa Misingi ya Ushirika Duniani pamoja, kutangaza shughuli zinazofanyika katika Vyama vya Ushirika na kuwataka Vyama vingi zaidi vya SACCOS vyenye Leseni kujiunga na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT) kuimarisha nguvu ya pamoja.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SCCULT, Dkt. Cuthbert Msuya, amesema Chama hicho kimeendelea kuvijengea uwezo Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji ikiwemo matumizi ya TEHAMA hususan Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) katika utoaji wa huduma kwa Wanachama, utunzaji wa taarifa, pamoja na uandaaji wa taarifa za Kifedha na kusisitiza kuwa SCCULT itaendelea kuwajengea uwezo Viongozi na Wanachama wake. 

Dkt. Cuthberth amesema malengo ya Jukwaa hilo ni kutoa nafasi kwa viongozi kujadili utendaji wa SACCOS, matumizi ya TEHAMA, Utawala Bora na Uongozi, kupitia Taarifa ya Utendaji wa SACCOS ya mwaka 2022, kubadilishana uzoefu ili kujadili na kuboresha utendaji wa SACCOS nchini.

Baadhi ya Mada zilizowasilishwa na wajumbe Wakachangia kwa Majadiliano ni pamoja na suala la ulinzi wa Mlaji (Consumer Protection Policy), mafunzo kwa wanachama wanaotarajia kustaafu ili kuwajengea uwezo wa kuendesha maisha ya ustaafu, Uwazi wa taarifa za mikopo hasa riba, Haki na Wajibu wa Wanachama, uelewa wa Vihatarishi vinavyoendana na huduma za bidhaa za mikopo (Risk), Afya ya Akili, na Utawala Bora. 

Akizungumza katika Jukwaa hilo, Mrajis Msaidizi - Huduma za Kifedha, CPA  Josephat Kisamalala,  ametoa rai kwa SACCOS kutathmni aina za mikopo wanayotoa na kujikita zaidi katika bidhaa ya Mikopo ambayo inaleta tija na manufaa zaidi kwa wanachama ambayo urejeshaji wa mikopo utakuwa rahisi na mwepesi kwa wanachama na kuleta faida zaidi kwa Chama pamoja na kusisitiza elimu ya Ushirika kwa Wanacha pamoja na Vyama kuwekeza katika Benki ya Ushirika ya KCBL.  

Wajumbe wa Jukwaa hilo wamesema ni muhimu Vyama hivyo kudhibiti na kuimarisha Usiri wa taarifa za Wanachama kwa mujibu wa miongozo ya ndani ya Chama ili kumlinda Mwanachama, kulinda rasilimali za Chama, kulinda fedha za Wanachama pamoja, utoaji wa taarifa kwa wanachama pamoja na kuzingatia taratibu za Uchaguzi wa Viongozi ili kupata viongozi bora.