Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amevitaka Vyama vya Ushirika kufanya Mikataba kwa uwazi kwa kuhusisha wadau husika na Mikataba hiyo ili kuepusha uwezekano wa Migogoro.

Dkt. Ndiege ametoa kauli hiyo wakati wa Mkutano na Wanaushirika wa utiaji Saini wa Mkataba kati ya  Ushirika wa Mradi wa Pamoja wa Murosang na Mwekezaji wa Mashamba, Kampuni ya McJaro Ltd akiwa katika ziara ya kikazi Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Machi 12, 2024.

Mrajis amesema Vyama vihusishe wadau na Wataalamu mbalimbali kwa kupata Ushauri na kuelewa Mikataba kabla ya kusaini ili kuepusha migogoro inayotokana na kutoelewa masharti ya baadhi ya vipengele vya Mikataba. Amesema kuwa Mikataba hiyo isainiwe kwa kuwaalika Wanachama na Wadau wa Chama kwa Uwazi na ikiwezekana iwe kwa lugha ya Kiswahili.

“Nitoe wito kwa Vyama msijifungie wenyewe peke yenu Mkaingia Mikataba bila kuwa na uelewa sahihi, iteeni Wataalamu pale mnapohitaji msaada na hata siku ya kusaini iteni Wanachama na Wadau washuhudie kama tunavyofanya leo hii,” alisema Mrajis.

“Kama Mkataba upo kwa lugha ya Kiingereza basi hakikisheni kuwa Mkataba huo pia ikiwezekana uwe katika lugha ya Kiswahili ili watu wauelewe na kama kuna jambo la ufafanuzi ulizeni na Ofisi yangu itawapa ushirikiano pale mnapouhitaji,” amesisitiza

Katika mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Hai, Mhe. Saashisha Mafuwe, ametoa rai kwa wanaushirika kuhamasisha vijana kuingia katika Vyama vya Ushirika ili kuwa na uendelevu wa Vyama na kuongeza kasi, tija na ustawi wa Vyama vyenye ubunifu na mwelekeo chanya kiuchumi.