Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amewataka Watumishi wa TCDC na watendaji wa Vyama vya Ushirika kutekeleza vipaumbele vya saba(7) vya Tume kama vilivyotolewa na Kamisheni ya Ushirika ili kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Ushirika.

"Hakikisheni mnavijua na kuvitekeleza Vipaumbele saba(7) vya Tume na kuvifanyia kazi ipasavyo kama vilivyotolewa na Kamisheni ya Tume, amesema Dkt. Ndiege.

Mrajis ameyasema hayo leo Disemba 22, 2023 katika Kikao cha tatu(3) cha Watumishi wote wa Tume wa Makao Makuu na Wawakilishi wa mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Dkt. Ndiege amevitaja Vipaumbele hivyo kuwa ni Uwekezaji katika Mifumo ya kisasa ya kidigitali; Kurahisisha Mchakato wa uanzishaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika; kuhamasisha Mfumo wa Ushirika kujiendesha kibiashara; Kuboresha Sera; Sheria na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika; Kuhamasisha Ushirika kwenye Sekta mbalimbali na makundi maalumu; Kuimarisha uwekezaji na Mali za Ushirika katika uzalishaji; na Kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza Sekta Ushirika.

Aidha, amesisitiza kuwa katika kutekeleza vipaumbele hivyo,viongozi wasiruhusu Watu kuchezea na kuharibu Mifumo ya Ushirika.

"Msiruhusu watu wachezee mifumo ya Ushirika (ikiwemo Mfumo wa MUVU) msiruhusu watu waharibu, nami katika hilo nitawaongezea nguvu," amesema Dkt. Ndiege.

Mrajis pia amewataka Watumishi kuwa waadilifu katika utendaji wa kazi na kutumia vizuri fedha zinazopelekwa kwa ajili ya Usimamizi wa Vyama ili kuleta mabadiliko chanya ya kisekta na Taifa kwa ujumla.

"Pamoja na mengine, tuna changamoto ya uaminifu, hili lazima tubadilike, hatuna nia ya kumuumiza mtu, tunahitaji uadilifu na jitahidini kuwa waadilifu katika kusimamia Vyama," amesema Mrajis.