Watoa Huduma katika Vyama vya Ushirika wametakiwa kutoa huduma kwa uwazi na ufasaha mkubwa pasipo kushawishiwa na vitendo vya rushwa na kwa kuzingatia Sera, Sheria na Kanuni za Vyama vya Ushirika.

Wito huo umetolewa na Mrajis wa Vyama vya ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege alipofungua Kikao Kazi cha Ofisi ya Mrajis na Watoa Huduma katika Vyama vya Ushirika kilichofanyika Jijini Dodoma leo, Aprili 06, 2022.

“Kwa kuwa Serikali imeweka Imani kubwa kwenu ili kuvihudumia Vyama vya Ushirika ambavyo ni vyombo vya wananchi wake ambao wengi wao ni wakulima. Toeni huduma zenu kwa uwazi na ufasaha mkubwa pasipo kushawishiwa na vitendo vya rushwa,” amesema Dkt. Ndiege.

Mrajis amewataka Watoa Huduma kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu dhana ya Ushirika na uendeshaji wake na kufuata Misingi ya Ushirika inavyoelekeza

“Hakikisheni kuwa huduma zenu zinatolewa kwa wakati stahiki kulingana na mikataba yenu na Vyama. Mfano, wakati mmekubaliana kukusanya madeni au kufunga mtandao wa TEHAMA, hakikisheni huduma hizo zinatolewa kwa wakati na sio kuachia kazi njiani,” amesema Dkt. Ndiege.

Aidha, Mrajis amewataka Watoa Huduma katika kutekeleza majukumu yao kwa Vyama vya Ushirika kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Warajis Wasaidizi na Maafisa Ushirika waliopo katika maeneo husika ili kuimarisha udhibiti wa huduma wanazozitoa kwa Vyama vya Ushirika, na pia kuweza kutambulika.

“Vyama vyetu vya Ushirika vipo katika maeneo mbalimbali yaani mijini na vijijini, na wote hawa ni Watanzania ambao wanatamani vyombo vyao vipige hatua ya kimaendeleo. Hivyo hamna budi kuhakikisha kuwa hamfungamani pekee na aina fulani ya vyama vya ushirika mfano SACCOS zilizopo mijini pekee mkasahau zile za vijijini. Toeni huduma zenu pasipo upendeleo,” amesema Mrajis.