Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema hivi sasa Sekta ya Ushirika inakwenda vizuri kwq kuongeza tija ya Maendeleo katika ustawi wa Wananchi wengi nchini.

Rais Mhe.Dkt. Samia amesema hayo wakati wa Uzinduzi wa Benki ya Ushirika uliofanyika leo Aprili 28, 2025 Jijini Dodoma.

Rais amesema Ushirika sasa una mwelekeo mzuri kutokana na Vyama vya Ushirika kuwa na msukumo chanya wa kuendeleza shughuli za uchumi hadi kufikia hatua ya kuchangia Mtaji wa kuanzisha Benki ya Ushirika ambayo inamilikiwa na Wanaushirika kwa asilimia 51 na Mtaji wa Shillingi Billioni 58. 

Aidha, Benki hiyo inaanza ikiwa tayari na matawi manne katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Mtwara na Tabora; pamoja na mawakala 58 ambao wanatokana na Vyama Vikuu vya Ushirika nchini.

Mheshimiwa Rais ametoa rai kwa Benki hiyo kuwa chachu ya kuwafikia Wakulima na Wananchi wengi vijijini kupitia mikopo itakayotolewa. Pamoja na mambo mengine, ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuendelea kuimarisha usimamizi wa Vyama ili vijiendeshe kibiashara, kutumia Mifumo ya TEHAMA na Mahesabu yasomwe kwa wakati.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wanaushirika, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za Kifedha, Wabunge, Vyama vya Siasa pamoja na Wakazi wa Jiji la Dodoma.