Kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa saba inayolima zao la Pamba hapa nchini pamoja na Wakuu wa Wilaya, Wabunge, viongozi wa vyama vikuu vya ushirika na Wadau wa Pamba nchini kimefanyika tarehe 13 Desemba, 2022 Mjini Musoma katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee ameeleza kikao hicho ni muhimu kwa maendeleo ya kilimo cha zao la pamba hapa nchini.
Mheshimiwa Mzee amesema kuwa Mkoa wa Mara una Vyama vya Ushirika vya msingi 235 ambavyo vinajishughulisha na ukusanyaji na uuzaji wa pamba na Vyama Vikuu vya Ushirika viwili ambapo kimoja kinaratibu biashara ya Pamba.
Akizungumzia uzalishaji wa pamba katika Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa Mwaka 2022/2023 Mkoa ulizalisha kilo 6,458,000 za pamba zenye thamani ya shilingi 9,687,000,000 na msimu ujao wa mwaka 2023/2024 Mkoa wa Mara unalenga kuzalisha kilo 7,079,825 za pamba.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidigitali kwenye shughuli za kilimo unaenda kuongeza usimamizi, ufanisi na upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya mipango na bajeti ya uendelezaji wa Sekta ya Kilimo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mara ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika na taasisi zote zilizoratibu kikao kazi hicho kwa kufikiria usimamizi wa mavuno ya Pamba wakati huu kukiwa na muda bado wa kuendelea kutoa elimu kwa wakulima na viongozi wa Vyama vya Ushirika kuhusu mifumo inayopendekezwa.
Wakuu wa mikoa mingine walioshiriki katika kikao hicho ni kutoka mikoa ya Simiyu, Geita, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Mara na Katavi. Viongozi hao wamesema kikao hicho ni muhimu katika kuzungumzia na kupanga namna bora ya kuimarisha mnyororo wa uzalishaji na masoko ya zao la Pamba hapa Nchini.
Viongozi wengine walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Wabunge, Wakuu wa Wilaya, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala.