Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imeamua kumuunganisha mkulima na mnunuzi pamoja  kwenye Vyama vya Ushirika vya wakulima kwa lengo la kuwawezesha wanunuzi kushindana bei kwenye minada na hivyo kupandisha bei za mazao ya Mkulima.

"Tumeshuhudia mara kadhaa bei ya Korosho ikipanda kwasababu kuna Ushirika wa Mkulima, na mnunuaji moja kwa moja, hivyo tumemuondoa mtu wa kati ambao walikuwa wanakwenda moja kwa moja kununua mazao shambani na wananunua kwa bei ndogo," amesema Mhe. Rais Samia.

Dkt. Samia ameyasema hayo  Septemba 7, 2023 katika Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) wakati akijibu maswali kutoka Kwa wadau kwenye mkutano uliohusisha vijana ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua ambazo Serikali inazichukua kuondoa changamoto ya soko kwa wakulima.

“Tumeshuhudia hivi karibuni zao la Ufuta kwasababu tumeingiza kwenye Ushirika na tumetumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, wakulima wanapeleka mazao yao huko kwenye Ushirika , wanunuaji wanashindanishwa bei inapanda,”amesema Mhe. Rais Samia.

Mhe. Rais Samia amesema  katika zao la Mbaazi ambalo miaka miwili, mitatu nyuma  wakulima walihamasishwa walime sana na wakalima lakini kwasababu Wakulima hawakuunganishwa na soko na hawakuwa na mipango mizuri Mbaazi zilianguka bei sana na kuwavunja moyo wakulima. 

“Mwaka jana (2022) mbaazi iliuzwa kwa Sh.300 kwa kilo lakini mwaka huu (2023) wakulima wameuza kwa zaidi ya Shilingi 2,000 kwa kilo. Sasa huu ndio mtindo tutakaokwenda nao kwenye mazao mengine pia ili kumuunganisha mkulima na soko,” amesema Mhe. Rais.